Duru za mbio za vigari kuongezwa hadi 14

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, November 20  2017 at  17:27

Kwa Muhtasari

BAADA ya msimu wa kufana wa Mbio za kitaifa za vigari vya Autocross za msimu 2017, waandalizi Shirikisho la Mbio za Magari za Kenya (KMSF) wanapanga kuongeza duru kutoka tisa hadi 14 mwaka 2018.

 

Habari kutoka shirikisho hilo zinasema kwamba idadi kubwa ya washiriki katika raundi zote tisa imevutia Benki ya KCB na kuifanya kuwa tayari kuongeza udhamini kutoka Sh10 milioni walizomwaga mwaka 2017.

“Wadhamini wamefurahia sana washiriki kujitokeza kwa wingi kushindana na sasa wako tayari kuongeza kitita walichotoa mwaka 2017 ili duru zaidi ziongozwe. Kuna uwezekano mkubwa msimu ujao utajumuisha duru 14,” mdokezi wa kuaminika kutoka benki hiyo aliambia Swahili Hub mnamo Novemba 20, 2017.

Katika msimu uliokamilika Novemba 19, 2017, Hamza Anwar aliibuka mshindi baada ya kumaliza duru ya tisa na ya mwisho katika nafasi ya pili kwenye bustani ya Champagne katika kaunti ya Kajiado.

Anwar alijawa furaha baada ya kutawazwa mfalme wa mwaka 2017. “Ilikuwa siku nzuri sana. Nashukuru Mungu kwa kuniwezesha kutwaa ubingwa. Nasubiri kwa hamu kubwa msimu ujao,” alisema dereva huyo.

Rehan Shah alimaliza kitengo cha 4WD Turbo katika nafasi ya kwanza licha ya kushikilia nafasi ya pili nyuma ya Alfir Khan katika raundi ya tisa. Gillian Bailey na Ryan Bailey pia walishinda vitengo vyao.