Dylan Kerr apewa siku 7 kulipa faini ya Sh2,500 kwa kuvunja kiti

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  20:57

Kwa Muhtasari

KOCHA wa Gor Mahia, Dylan Kerr ametozwa faini ya Sh2,500 kwa kosa la kuvunja kiti cha plastiki katika mechi ya Ligi Kuu ya KPL iliyowakutanisha na Mathare United katika uwanja wa Manispaa ya Thika mnamo Oktoba 14, 2017.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni ya KPL ambayo ni waendeshaji rasmi wa kivumbi cha Ligi Kuu ya humu nchini, Kerr alizua vurugu katika mchuano huo na hatua yake ya kuvunja kiti ilikosa kudhihirisha sifa za uanaspoti alizotarajiwa kuonesha.

Ikitoa adhabu hiyo, KPL ilisisitiza kwamba Kerr ana jumla ya siku saba kulipia faini hiyo ya Sh2,500.

Isitoshe, mkufunzi huyo mzawa wa Uingereza alionywa kwamba huenda akaadhibiwa zaidi katika siku zijazo iwapo atayarudia makosa aliyoyadhihirisha katika mchuano huo uliowakutanisha vijana wake na mabingwa hao wa KPL 2008.

Ingawa Kerr alikiri kosa na kuomba radhi, KPL ilitilia mkazo suala la kuadhibiwa kwa kocha huyo kuwa litakuwa funzo kwa wakufunzi wengine.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Kerr kupoteza akidhibiti mikoba ya Gor Mahia msimu huu tangu kubanduka kwa kocha mzawa wa Brazil, Jose Marcelo Ze Maria.