http://www.swahilihub.com/image/view/-/4925584/medRes/2218044/-/15cv5sqz/-/cesc.jpg

 

Fabregas amuachia maumivu Hazard

Cesc Fabregas 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  09:40

Kwa Muhtasari

Fabregas ni mchezaji mwenye kiwango bora duniani

 

 

London, England. Edin Hazard ametaja Cesc Fabregas ni mchezaji wa aina yake aliyewahi kumuona katika medani ya soka duniani.

Hazard alisema Fabregas ni mchezaji mwenye kiwango bora duniani na alifurahi kucheza naye katika kikosi cha Chelsea.

Nahodha huyo wa Ubelgiji, alisema kiungo huyo alikuwa rafiki wa kweli na atamkumbuka kwa mchango mzuri aliotoa kwa miaka miwili aliyocheza Chelsea.

“Miaka mitano iliyopita niliwahi kusema ndoto yangu ni kucheza na Cesc Fabregas, ndani ya mwaka mmoja tu tulitwaa mataji mawili,” alisema Hazard.

Hazard alitoa kauli hiyo alipokuwa akimuga Fabregas (31) ambaye alicheza mchezo wa mwisho juzi usiku wa Kombe la FA dhidi ya Nottingham Forest kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Idadi kubwa ya wachezaji wa Chelsea walitokwa machozi baada ya Fabregas kuwaaga ndani ya vyumba vya kuvalia nguo.

Fabregas amecheza mechi 501 za mashindano ya Ligi Kuu England katika klabu mbili tofauti Arsenal na Chelsea.

Kiungo huyo nguli anatarajiwa kujiunga na Monaco ya Ufaransa akimfuata nahodha wake wa zamani katika kikosi cha Arsenal, Thierry Henry anayeinoa timu hiyo.

Licha ya kukosa mkwaju wa penalti kipindi cha kwanza, Chelsea ilitoka uwanjani kwa ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Alvaro Morata.

Fabregas alijiunga na Chelsea akitokea Barcelona Juni 2014 na kuipa mataji mawili ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Kombe la FA. Nguli huyo amecheza mechi 135 na amefunga mabao 15 katika kikosi hicho.