http://www.swahilihub.com/image/view/-/4918118/medRes/2213113/-/l6mi1l/-/kichapo.jpg

 

Floyd Mayweather alamba Sh20.7bil kwa dakika mbili

Floyd Mayweather (kulia) akimtembezea kichapo Tenshin Nasukawa 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, January 2  2019 at  09:49

Kwa Muhtasari

Mayweather hakutaka kuremba, alimmaliza mapema tu mpinzani wake

 

Tokyo, Japan. Bondia Floyd Mayweather hapigani kizembe. Anachoangalia wapi atapiga pesa ndefu ndipo anavaa glovu na kupanda ulingoni.

Juzi usiku alipanda ulingoni nchini Japan katika pambano lake na mcheza kikiboksi, Mjapani, Tenshin Nasukawa na alitumia dakika mbili tu kummaliza Mjapan huyo na kuvuta pesa yake kiulaini kabisa.

Kwa kumtwanga Nakasuwa, Mayweather, aliingiza Dola9 million (Sh20.7bilioni), alimpeleka chini mara tatu katika raundi ya kwanza na pambano likasimamishwa zikiwa zimesalia sekunde 40 kumaliza raundi hiyo.

Mpambano huo uliofanyika Saitama, Japan, ulikuwa wa raundi tatu, lakini Mayweather hakutaka kuremba, alimmaliza mapema tu mpinzani wake.

Nasukawa, ambaye hajawahi kupigwa, alianza vizuri lakini sekunde ya 70 akapelekwa chini baada ya kupata konde moja matata la mkono wa kushoto la Mayweather.

Dogo huyo wa miaka 20 alipigwa ‘uppercut’ moja na Mayweather sekunde 40 tangu aangushwe na akaenda chini kwa mara nyingine.

Mayweather alimuunganishia ngumi mfululizo Nasukawa kabla ya kumwangusha kwa mara ya tatu na safari hii aliokolewa na mwamuzi.

Ushindi huo unafanya Mayweather kufikisha rekodi ya mapambano 50-0 na alisema baada ya mpambano huo kuwa anajifurahisha na ameshastaafu ngumi.

“Huu huwezi kusema ni ushindi wa aina yake, ulikuwa mwepesi sana’ alisema bondia huyo. ‘Hata hivyo, sijapoteza mchezo.

Ni bondia mzuri na anapigana vizuri. Lakini nasema nimeshastaafu, Sina mpango wowote wa kurudi kwenye ngumi. ‘Nimekuja kwa ajili ya kuwafurahisha Watu wa Japan.’