GOtv yatia kikomo mkataba wa kipute cha GOtv

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:06

Kwa Muhtasari

AFISA Mkuu wa Mawasiliano wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Barry Otieno amesema kampuni ya GOtv imethibitisha kutorefusha kandarasi yao ya kudhamini kipute cha GOtv mwakani, hatua ambayo imewachochea kumfungulia milango mfadhili mpya.

 

Chini ya Sam Nyamweya, FKF iliwapa GOtv udhamini wa FKF Cup mnamo 2013 pamoja na kuwapokeza haki za kukiita kipute hicho ‘Ngao ya GOtv’.

Hata hivyo mkataba huo uliorasimishwa kwa kipindi cha miaka mitano sasa umetamatika na shirikisho kwa sasa linatafuta mdhamini mpya wa taji hilo kwa msimu wa 2018 na baadaye.

Mabingwa mara 13 wa taji la KPL, AFC Leopards waliingia katika mabuku ya historia mwishoni mwa wiki jana kwa kuwa kikosi cha kwanza kutia kapuni ubingwa wa Ngao ya GOtv mara mbili katika historia ya kipute hicho.

Leopards waliwapepeta Kariobangi Sharks 2-0 katika fainali iliyowakutanisha katika uwanja wa MISC Kasarani mnamo 2017.

Ingwe walitawazwa mabingwa wa makala ya kwanza ya GOtv mnamo 2013 baada ya kuwazidi maarifa Gor Mahia.
Mafanikio yaliyovunwa mwa Leopards katika msimu huo wa 2013 yalitosha kuwapa nafasi ya kudhihirisha ukubwa wa ubabe wao katika soka ya kimataifa baada ya kufuzu kushiriki Kombe la Mashirikisho (CAF Confederations Cup).

Hata hivyo, walibanduliwa mapema katika kivumbi hicho baada ya kunyukwa jumla ya mabao 4-2 na kikosi cha Supersport kinachoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Sofapaka ambao walitawazwa mabingwa wa KPL mnamo 2009 walinyanyua Ngao ya GOtv mnamo 2014 huku Bandari wakitia kapuni taji hilo mnamo 2015.

Washindi mara 11 na mabingwa watetezi wa KPL, Tusker walinyakua Ngao ya GOtv msimu jana baada ya kuwazidi maarifa Ulinzi Stars uwanjani Nyayo mnamo Oktoba 20, 2016.

Mbali na kujikatia tiketi ya kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Kombe la Mashirikisho, Leopards walitia kapuni kima cha Sh2 milioni msimu huu kutokana na ushindi wao wa GOtv.