http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119568/medRes/2346509/-/cdklwyz/-/geita+pic.jpg

 

Geita Gold yajiweka patamu

Na Saddam Sadick, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  11:33

 

Mwanza. Geita Gold imejiweka katika nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuilaza Mlale FC katika mchezo wa kusaka timu ya kupanda msimu ujao.

Timu hiyo ilishinda mabao 3-0 kwenye Ligi Ndogo ya mchujo matokeo yameiweka katika mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu.

Akizungumza jana, Kocha wa Geita Gold, Hassan Banyai alisema bado ana kazi ngumu mbele yake ya kushinda mechi ya marudiano ugenini.

Timu hiyo ya mkoani Geita ilimaliza Ligi Daraja la Kwanza katika nafasi ya tatu kwenye Kundi B ikiwa na pointi 42, huku Mlale ikimaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 39 Kundi A.

Katika ligi hiyo ya mchujo inazishirikisha timu nne zilizoshika nafasi mbili za juu zitacheza ligi nyingine dhidi ya timu za Ligi Kuu zitakazomaliza katika nafasi ya 17 na 18 ili kupanda Ligi Kuu.

Banyai alisema baada ya ushindi huo mnono katika mechi ya kwanza, anawaandaa wachezaji wake kuhakikisha wanashinda mchezo wa marudiano Aprili 22.

Kocha huyo alisema bado ndoto zao za kucheza Ligi Kuu hazijaisha, hivyo ni muda sasa wa kupambana katika ligi hiyo ya mchujo kuhakikisha wanafanya kweli na kufikia malengo yao.

“Kwanza tunashukuru kwa ushindi huu, bado tuna safari ngumu lakini hatuna budi kulinda matokeo haya kwenye mchezo wa marudiano ugenini, tumejipanga kutimiza ndoto yetu,” alisema Banyai.

Aliongeza anaamini mchezo wa marudio utakuwa mgumu kutokana na wapinzani kuhitaji kupindua matokeo wawapo nyumbani, hivyo watajitahidi kuhakikisha hawafanyi makosa.

“Kikubwa ni maombi na sapoti kwa mashabiki wetu,tunataka msimu ujao Mkoa wa Geita uwe na timu ya Ligi Kuu,tutajipanga kadiri tuwezavyo,”alisisitiza kocha huyo.