Gor mbioni kurefusha mikataba ya mastaa

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:04

Kwa Muhtasari

WANAPOJIANDAA kwa kampeni za kutetea ubingwa wa taji la KPL msimu ujao pamoja na kusuka upya kikosi kitakachowapigisha hatua kubwa zaidi katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (CAF Champions League) mnamo 2018, Gor Mahia wameanza harakati za kurefusha kandarasi za wachezaji nyota kambini mwao.

 

Afisa Mkuu Mtendaji wa miamba hao wa soka ya humu nchini, Omondi Aduda amekiri kwamba tayari mafowadi Jacques Tuyisenge na Meddie Kagere pamoja na kiungo Ernest Wendo wametia saini mikataba mipya ya miaka mitatu kila mmoja katika maelewano yatakayowadumisha kambini mwa Gor Mahia hadi 2020.

Aduda ameapa pia kuanzisha mazungumzo rasmi na wachezaji wengine watatu ambao wana mikataba itakayokuwa imetamatika kufikia mwishoni mwa Februari 2018.

Kandarasi kati ya Gor Mahia na fowadi George ‘Blackberry’ Odhiambo inatamatika rasmi kufikia Desemba 31, 2017.

Masogora wengine ambao wapo katika hatari ya kukosa kunogesha kampeni za Gor Mahia katika michuano ya KPL msimu ujao pamoja na mechi za kimataifa za kuwania taji la Klabu Bingwa barani Afrika ni pamoja na beki Harun Shakava, difenda mzawa wa Uganda Godfrey Walusimbi na nahodha Musa Mohamed.

Kandarasi kati ya Blackberry na Gor Mahia inatamatika mnamo Desemba 31, 2017 huku muda wa kuhudumu kwa Shakava kambini mwa wapambe hao wa soka ya humu nchini ukitarajiwa kufikia ukingoni mnamo Januari 14, 2018. 

Kandarasi za Musa na Walusimbi na waajiri wao zinafikia tamati mnamo Januari 15 na Januari 22, 2017 mtawalia.