Gor yapanga kuanzisha tuzo za kila mwezi

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:25

Kwa Muhtasari

MABINGWA mara 15 wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia wamepanga kuwaiga Sofapaka na kuanzisha tuzo za kila mwezi kwa wachezaji wao ili kuimarisha viwango vya ushindani miongoni mwa nyota wanaokikamilisha kikosi hicho.

 

Kwa mujibu wa Judith Anyango ambaye ni Mratibu Mkuu kambini mwa magwiji hao wa soka ya humu nchini, tuzo za aina hiyo zitachangia pakubwa kudumisha hamasa ya wachezaji ambao wanatawaliwa na kiu ya kutawazwa wafalme wa KPL kwa mara nyingine msimu huu.

“Gor Mahia wamekuwa wakifanya vyema katika kampeni za KPL tangu kikosi kipate wadhamini wa kudumu. Hatua ya kutuzwa kwa wachezaji ni moja kati ya mbinu na mikakati itakayowachochea vijana kujituma zaidi na hatimaye kusajili matokeo ya kuridhisha katika kila mchuano uliopo mbele yao,” akasema Anyango.

Kulingana na kinara huyo, tuzo za kila mwaka zitafanya Gor Mahia kuwa kivutio kikubwa zaidi ndani na nje ya Kenya hasa ikizingatiwa upekee na ukubwa wa mchango wa juhudi hizo katika kuwapa motisha wachezaji.

Isitoshe, anaamini kuwa tuzo za nui hiyo zitawachochea vinara wa KPL pamoja na wale wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuboresha zaidi zawadi wanazozitoa kila mwishoni mwa msimu kwa klabu na wachezaji wanaosajili matokeo ya kuridhisha zaidi.

Akisisitiza kwamba tuzo hizo zitaanza kutolewa rasmi mwakani, Anyango amesema kuwa kwa sasa usimamizi wa Gor Mahia unashiriki mazungumzo na benchi la kiufundi pamoja na wachezaji wa kikosi hicho kubainisha vitengo vya kutuzwa, kiwango cha tuzo na aina za tuzo zitakazotolewa kwa kila kitengo na kwa idadi ipi ya wachezaji.

“Tunashauriana na wadau mbalimbali kuhusu aina za tuzo za kutolewa, viwango vya tuzo zenyewe na vitengo vya kutambuliwa kisha kuzawidiwa,” akasema.

Wakati uo huo, kocha Dylan Kerr ameapa kurejeshea hadhi ya klabu hiyo ambayo ilipoteza taji la KPL msimu jana baada ya kuzidiwa maarifa na Tusker waliotia kapuni ubingwa wa KPL kwa mara ya 11 chini ya kocha Paul Nkata ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Bandari.