http://www.swahilihub.com/image/view/-/4919688/medRes/2214213/-/8rers0/-/tambwe.jpg

 

Huku Tambwe kule Makambo patamu!

Amissi Tambwe 

Na ELIYA SOLOMON

Imepakiwa - Thursday, January 3  2019 at  12:16

Kwa Muhtasari

Naamini tunaweza kuendelea kufanya vizuri kwa kufunga na kuisaidia Yanga

 

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe amesema ushirikiano wake na Heritier Makambo anaamini unaweza kuifanya Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2018/19.

Tambwe ambaye amerejea kwenye makali yake ya ufungaji, alisema kilichomwondoa kwenye kasi yake ya ufungaji yalikuwa ni majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.

Mrundi huyo ana mabao matano huku pacha ambaye amekuwa akicheza naye kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga, Makambo akiwa na mabao 11 kwenye kilele cha orodha ya wafumania nyavu wa Ligi Kuu Bara.

“Kikubwa ni kuisaidia timu kuchukua ubingwa, tunaweza kucheza kwa pamoja kama kocha ataendelea kuona tunaendana, lakini binafsi nafurahia kucheza naye.

“Tukiwa washambuliaji wawili mbele inamaana tunakuwa na nguvu kubwa kwenye safu yetu ya ushambuliaji, naamini tunaweza kuendelea kufanya vizuri kwa kufunga na kuisaidia Yanga kuchukua ubingwa,” alisema Tambwe.

Mshambuliaji huyo ambaye amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, amepachika mabao yake hayo matano kwenye michezo dhidi ya Singida United, Tanzania Prisons ambapo alifunga mawili kwenye kila mchezo na moja dhidi ya Biashara United.

Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa na pointi 50, walizozikusanya kwenye michezo 18 ambayo wameshinda 16 na kutoka sare miwili.

Wanaofuata kwenye nafasi ya pili na tatu ni Azam wenye pointi 40.