http://www.swahilihub.com/image/view/-/4660654/medRes/2043122/-/ipmli5z/-/ligi.png

 

Idadi ya wageni Ligi Kuu itathminiwe kwa kina

 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  10:21

Kwa Muhtasari

Kila nchi bado inatumia utaratibu unafaa kwa mazingira yake

 

Katika mitandao ya kijamii kuna barua inasambaa kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina mpango wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni katika vilabu kutoka saba hadi 10 kwa lengo la kuongeza ushindani na hivyo kukuza kiwango cha wachezaji wa ndani.

Barua hiyo ni matokeo ya mjadala wa muda mrefu kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye Ligi Kuu ya Bara na Ligi Daraja la Kwanza ambako klabu sasa zinatumia wachezaji wengi wa kigeni kutokana na kanuni kuruhusu wachezaji saba.

Bado suala hilo halijapitishwa rasmi na vyombo vya uamuzi vya TFF na kama vitakuwa vimepitisha, basi itakuwa ni jana jioni. Hata hiyo, tunalazimika kuzungumzia suala hilo kutokana na unyeti wake na jinsi linavyoweza kuwa na matokeo chanya au hasi katika mpira wa miguu nchini.

Pengine kuna sehemu nyingi duniani zinazoruhusu idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni na wakati fulani Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) liliwahi kutaka kuingilia kati na kupendekeza kiwango cha 6:5, yaani wachezaji wanaocheza uwanjani wawe sita wazalendo na watano wageni kwa klabu zenye uwezo.

Kutokana na kuwepo kwa sheria tofauti za ajira na ushirikiano wa kikanda suala hilo limeshindikana na hivyo kila nchi bado inatumia utaratibu ambao unafaa kwa mazingira yake.

Kwa mfano, kwa nchi za Umoja wa Ulaya (EU), suala hilo ni rahisi kwa sababu wananchi wa mataifa yanayounda EU yanachukulia wananchi wake kuwa raia wa umoja huo bila ya kutaja nchi zao.

Hivyo, mchezaji kutoka Ufaransa anacheza Hispania kama mwananchi wa nchi hiyo kwa kuwa ana uraia wa EU na hivyo katika masuala ya ajira anakuwa na haki sawa na raia wa Hispania. Ndio maana klabu za nchi za EU klabu zinaweza kuwa na wachezaji wote kumi na moja wanaoanza mechi kutoka nje ya nchi.

Sheria zao za kazi zinaruhusu raia wa nchi moja kwenda kufanya kazi nchi nyingine mwanachama wa EU bila ya masharti ya kupata kibali cha kazi.

Utaratibu wa huku ni tofauti. Bado raia wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini) hawawezi kufanya kazi Tanzania wakiwa na haki zote za uraia.

Lakini kikubwa zaidi ni mipango ya maendeleo ambayo TFF imejiwekea. TFF bado haijaweza kuzilazimisha klabu kuwa na programu za kukuza kimpira watoto wadogo, vijana na wanawake. Pamoja na kanuni kutaka klabu ziwe na timu za vijana, utekelezaji wa suala hilo bado unafanywa kwa kubabaisha. Ni timu chache ambazo ukizikurupusha kwa kuzitaka zionyeshe timu zake za vijana zitaweza kufanya hivyo.

Klabu nyingi zinakusanya timu za vijana pale zinapotakiwa mashindanoni tu na baada ya hapo timu hizo hupotea. Hakuna programu za mafunzo kwa vijana na hakuna sera zinazoongoza uendeshaji wa timu hizo.

Katika mazingira kama hayo, huwezi kuruhusu idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ili kuongeza ushindani kwa wachezaji wa nyumbani, wakati huna programu za kuendeleza vijana wazalendo. Ni lazima TFF iwe na uwezo wa kuzilazimisha klabu zetu kuwa na timu za watoto na vijana kabla ya kuruhusu idadi kubwa ya wachezaji kutoka nje.

Ni vizuri TFF na Serikali zikaangalia suala hili kwa makini na kama kuna mpango huo, usitishwe mara moja ili kuandaa mazingira mazuri kwanza.