http://www.swahilihub.com/image/view/-/4186608/medRes/1809390/-/43uuf9z/-/italia.jpg

 

Italia nje ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 60

Gianluigi Buffon

Golikipa Gianluigi Buffon wa Italia baada ya mchuano wa kufuzu Kombe la Dunia Mwaka 2018 kati ya Italia na Uswidi mnamo Novemba 13, 2017 uwanjani San Siro mjini Milan. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  16:08

Kwa Muhtasari

Kipa Gianluigi Buffon amestaafu kutoka timu ya taifa ya Italia baada ya Uswidi kufungia miamba hao nje ya Kombe la Dunia mwaka 2018 hapo Novemba 13, 2017.

 

KIPA Gianluigi Buffon amestaafu kutoka timu ya taifa ya Italia baada ya Uswidi kufungia miamba hao nje ya Kombe la Dunia mwaka 2018 hapo Novemba 13, 2017.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka 1958 Italia itakosa Kombe la Dunia.

Italia, ambayo iliibuka bingwa mwaka 1934, 1938, 1982 na 2006, ilibanduliwa nje ya safari ya kufika Urusi kwa jumla ya bao 1-0.

Bao lililozamisha chombo cha Italia lilifungwa na kiungo mkabaji Jakob Johansson katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Novemba 10 nchini Uswidi. Mechi ya mkondo wa pili iliishia sare tasa mijini Milan mnamo Novemba 13.

Baada ya mechi hiyo, Buffon, 39, ambaye amechezea timu ya Italia miaka 20, alitangaza kustaafu kwake. “Ni aibu kubwa kuwa mechi yangu ya mwisho imesadifiana na Italia kushindwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia.”

Italia ndio timu pekee imewahi kushinda Kombe la Dunia ambayo itakosa makala yajayo nchini Urusi.

Brazil, ambayo inajivunia mataji mengi (1958, 1962, 1970, 1994, 2002), ilikuwa timu ya kwanza kujikatia tiketi ya kuelekea Urusi. Ujerumani, ambayo ilinyakua mataji ya mwaka 1954, 1974, 1990 na 2014, pamoja na mabingwa wa mwaka 1978 na 1986 Argentina, mabingwa wa mwaka 1930 na 1950 Uruguay, Ufaransa (1998), Uingereza (1966) na Uhispania (2010) walifuzu.

Mataifa mengine yaliyoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2014 yatakayokosa kindumbwendumbwe cha mwaka 2018 ni Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast, Marekani, Bosnia & Herzegovina, Ugiriki, Uholanzi, Ecuador na Chile.

Eneo la Oceania lina nafasi ya kupata tiketi mbili zilisalia ambapo Australia italimana Honduras jijini Sydney nayo Peru itakuwa nyumbani kuzichapa dhidi ya New Zealand mnamo Novemba 15. Washindi wa mechi hizi mbili watakamilisha orodha ta mataifa 32 yatakayowania taji nchini Urusi.

Droo ya mwisho ya Kombe la Dunia itafanywa Desemba 1 mwaka 2017 jijini Moscow, Urusi.        

 

Orodha ya mataifa yaliyofuzu:

Bara Ulaya

Urusi (wenyeji)

Ubelgiji

Ujerumani

Uingereza

Uhispania

Poland

Iceland

Serbia

Ureno

Ufaransa

Uswizi

Croatia

Uswidi

 

Amerika Kusini

Brazil

Argentina

Uruguay

Colombia

 

Bara Afrika

Nigeria

Misri

Senegal

Morocco

Tunisia

 

Bara Asia

Iran

Japan

Korea Kusini

Saudi Arabia

 

Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean

Mexico

Costa Rica

Panama