Je, Uganda itatetemesha Raga za Afrika nyumbani?

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  16:44

Kwa Muhtasari

UGANDA watakuwa na shinikizo nyumbani Raga za Afrika za wachezaji saba kila upande zitakapoanza jijini Kampala mnamo Oktoba 6, 2017.

 

Waganda waliibuka washindi mwaka 2016 kwa kupepeta Namibia 38-19 katika fainali uwanjani Kasarani wakati Kenya ilikuwa mwenyeji.

Makala ya mwaka huu yamevutia mataifa 10, lakini Kenya haishiriki kwa sababu ililinda nafasi yake katika Kombe la Dunia kwa kumaliza ya nne nchini Urusi mwaka 2013.

Baada ya mashindano haya ya siku mbili ya Afrika kukamilika, mshindi na nambari mbili watajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Marekani.

Wataungana na Kenya, Afrika Kusini, Marekani, Canada, Argentina, Uingereza, Ufaransa, Wales, Scotland, Jamhuri ya Ireland, Urusi, Australia, Fiji, Samoa na mabingwa watetezi New Zealand.

Timu mbili za kwanza kutoka Afrika pia zitaingia katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2018 nchini Australia.  

Kwingineko, Shirikisho la Raga duniani (World Rugby) limetengea Kenya tiketi 40 za Kombe la Dunia la raga ya wachezaji saba kila upande litakalofanyika mjini San Francisco nchini Marekani mwaka 2018.

Tiketi hizo, ambazo ni za siku tatu za mashindano (Julai 20-22, 2018), zinauzwa kati ya Sh32, 817.60 na Sh45, 511.20 kila moja.

Shujaa ya Kenya haishiriki Kombe la Afrika kwa sababu ilifuzu kushiriki Kombe la Dunia moja kwa moja katika kitengo cha wanaume baada ya kumaliza makala yaliyopita katika nafasi ya nne nchini Urusi mwaka 2013.

Lionesses ya Kenya haikufuzu kushiriki Kombe la Dunia la wanawake ambalo pia litaandaliwa mjini San Francisco mwaka 2018.

 

MAKUNDI (MWAKA 2017):

A – Uganda, Tunisia, Morocco, Zambia, Ghana

B – Madagascar, Zimbabwe, Senegal, Botswana, Mauritius

 

MSIMAMO (MWAKA 2016):

1. Uganda

2. Namibia

3. Kenya

4. Madagascar

5. Zimbabwe

6. Tunisia

7. Nigeria

8. Morocco

9. Senegal

10. Botswana

11. Zambia

12. Mauritius