http://www.swahilihub.com/image/view/-/5128062/medRes/518816/-/c1s8u6z/-/mchongo+pic.jpg

 

Jella aipa mchongo Taifa Stars

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Thursday, May 23  2019 at  11:50

 

Dar es Salaam. Nahodha wa Taifa Stars iliyoshiriki Fainali za Afrika (Afcon) mwaka 1980, Jellah Mtagwa amewataka nyota wa sasa wa Stars kujituma, kuwa na umoja na kujitoa kwa Taifa ili wafanye vizuri kwenye fainali za mwaka huu.

Jellah ambaye amekuwa nahodha wa Stars kwa miaka 10 tangu 1974 alibainisha hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, nyumbani kwake Dar es Salaam.

Alisema nafasi ambayo Stars imeipata ni nyeti katika soka la Afrika, hivyowachezaji wasifikirie watapata nini kwenye hayo mashindano, bali wafikirie Taifa litakuwa katika hali gani watakaposhinda.

"Wakati wetu tulijitoa sana, wachezaji kila mmoja alionyesha uchu wa kutaka mafanikio, hatukuwaza malipo, tulitaka heshima.

"Hata tulipofungwa kwenye Afcon, matokeo hayakutuumiza mno, sababu tulicheza na wenyeji Nigeria wakatufunga 3-1, Ivory Coast tukatoka nao sare na Misri wakatufunga, lakini mpira tulicheza," anasema.

Beki huyo tegemeo wa zamani wa Starsm Pan African na Yanga alisema mashindano ya Afrika ni mashindano magumu, ambayo yanahitaji umakini, uwezo na kujituma ili kufanya vizuri.

"Ni mashindano magumu na timu za kundi letu ni ngumu, Stars wanapaswa kugangamala haswa ili wasije kuishia hatua ya makundi au kuwa timu itakayofungwa mabao mengi," alisema Jellah.

Alisema wasiwasi wake ni kuchelewa kuanza maandalizi kwa Stars mpaka sasa kwani kipindi hiki timu ilipaswa kuanza mazoezi ya pamoja.

"Wanahitaji kucheza mechi nyingi za kirafiki, lakini pia kufanya mazoezi ya pamoja kwa muda kidogo, kipindi hiki ilipaswa Ligi yetu iwe imekwisha na timu imeanza kujiandaa kwa Afcon," alisema Jella.