KCB yapata ushindi wa tisa mfululizo ligi kuu raga

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Saturday, February 10  2018 at  19:51

Kwa Muhtasari

Klabu ya raga ya KCB imeandikisha ushindi wake wa tisa mfululizo kwenye Ligi Kuu baada ya kunyamazisha wenyeji wake Mombasa 60-0, Jumamosi.

 

KLABU ya raga ya KCB imeandikisha ushindi wake wa tisa mfululizo kwenye Ligi Kuu baada ya kunyamazisha wenyeji wake Mombasa 60-0, Jumamosi.

Wanabenki hawa walivuna ushindi kupitia miguso ya Felix Ojow, Michael Kimwele, Marlin Mukolwe, Elphas Adunga, Stafford Abeka (miwili), Curtis Lilako, Darwin Mukidza na Edwin Otieno na mikwaju ya Essay Otieno na Mukidza.

Klabu zote ndani ya mduara wa tano-bora zilijizolea ushindi kila mmoja.

Homeboyz ilinyuka Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta 27-13, Kabras Sugar ikacharaza Kisii 47-15, Impala Saracens ikaliza Nakuru 43-36 nayo Kenya Harlequins ikazima Strathmore Leos 23-6.

Mwamba ndiyo timu pekee kutoka nje ya mduara wa tano-bora iliyoshinda. Mabingwa hawa wa mwaka 1985 walipepeta mabingwa mara 17 Nondescripts 53-12.

Kichapo hiki cha Nondies kinaiweka katika hatari zaidi ya kutemwa kutoka Ligi Kuu.

Zikiwa zimesalia mechi mbili msimu 2017-2018 kufikia tamati, Nondies inavuta mkia.