KPA ya Kenya yaandikisha ushindi wa kwanza katika mashindano ya Afrika ya mpira wa vikapu

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  17:06

Kwa Muhtasari

Mabingwa wa Ukanda wa Tano wa Afrika, Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA), wamesajili ushindi wa kwanza Jumanne katika mashindano ya mpira wa vikapu ya Afrika nchini Angola.

 

MABINGWA wa Ukanda wa Tano wa Afrika, Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA), wamesajili ushindi wa kwanza Jumanne katika mashindano ya mpira wa vikapu ya Afrika nchini Angola.

Miamba hao wa Kenya wamelaza Daring Club Motema Pembe (DCMP) kwa alama 70-51, siku mbili baada ya kufungua kampeni yao kwa kupepetwa 75-43 na wenyeji Primeiro de Agosto.

Dhidi ya DCMP kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, KPA ya kocha Anthony Ojukwu ilianza kwa kushinda robo ya kwanza 22-16.

Iliingia mapumzikoni ikiongoza 34-29 baada ya Wakongo hao kunyakua robo ya pili 13-12. Warembo wa Ojukwu hawakutaka mzaha katika robo mbili za mwisho walizonyakua 19-10 na 17-12, mtawalia.

Felmas Adhiambo Koranga alifungia KPA alama nyingi (19) naye Mukoso Nyoka akaongoza katika ufungaji wa pointi za DCMP (12).

Wawakilishi wengine wa Ukanda wa Tano katika mashindano haya ni Benki ya Equity ya Kenya.

Vimulimuli

Equity ya Kocha David Maina imekuwa ikiona vimulimuli pekee baada ya kulimwa 99-30 na InterClube ya Angola (Novemba 13), kulemewa 59-32 na GS Petroliers ya Algeria (Novemba 12) na kuzabwa 62-43 na First Bank ya Nigeria (Novemba 11).

Mabingwa wa Kenya, Equity, wako katika kundi A pamoja na GS Petroliers, First Bank, InterClube, na V-Club kutoka DR Congo.

Kundi B linaleta pamoja Agosto, Daring Club Motema Pembe, KPA, na Ferroviario Maputo kutoka Msumbiji.