KPL 2018 kuanza Februari 2

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, December 5  2017 at  12:54

Kwa Muhtasari

RATIBA ya Ligi Kuu ya Soka ya Kenya ya mwaka 2018, imetangazwa. Kampuni inayoendesha Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (KPL) imesema Jumatatu kwamba ligi itaanza Februari 2 baada ya shindano la Super Cup kati ya mahasimu wa jadi Gor Mahia na AFC Leopards hapo Januari 28 na kukamilika Novemba 10, 2018.

 

Kulingana na ratiba ilitolewa Desemba 4, 2017, Ligi Kuu itahusisha klabu 18. Klabu hizo ni Gor na Leopards, ambazo zilishinda ligi na kombe la GOtv Shield, mtawalia.

Washiriki wengine ni Ulinzi Stars, Zoo Kericho, Chemelil Sugar, Tusker, Nzoia Sugar, Kariobangi Sharks, Vihiga United, Mathare United, Sofapaka, Bandari, Posta Rangers, Wazito, SoNy Sugar, Kakamega Homeboyz na mshindi kati ya Thika United na Ushuru.

Vihiga na Wazito zimeingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kumaliza Ligi ya Supa katika nafasi mbili za kwanza mwaka 2017.

Mwaka 2017, ligi ilianza mwezi Machi baada ya vuta-nikuvute kati ya KPL na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuhusu idadi ya washiriki wa Ligi Kuu. KPL ilitaka klabu 16 nayo FKF ilisisitiza klabu 18.