Kivumbi cha KPL Top 8 chafutiliwa mbali msimu wa 2018

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:25

Kwa Muhtasari

KAMPUNI ya KPL ambayo huratibu na kuendesha kipute cha KPL Top8 kwa klabu zinazokamilisha kampeni za kila msimu ndani ya mduara wa nane-bora jedwalini, imefutilia mbali kivumbi hicho katika kalenda ya mashindano ya mwaka ujao wa 2018. 

 

Muhoroni Youth ndio waliotawazwa mabingwa wa kinyang’anyiro hicho katika msimu wa 2016 baada ya kuwazidi maarifa Gor Mahia ambao ni washindi mara 16 wa Ligi Kuu ya humu nchini. 

Kwa mujibu wa Jack Oguda ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL, kiini cha kutosakatwa kwa kivumbi cha Top 8 mwakani ni hatua ya kujiondoa kwa waliokuwa wadhamini wakuu wa michuano hiyo, SuperSport katika soka ya Kenya na kuyeyuka kabisa kwa matumaini ya mdhamini mbadala kupatikana.

“Kama hali ilivyokuwa 2017, itatulazimu kutoshiriki baadhi ya mapambano ya soka yaliyopangiwa kutandazwa katika mwaka wa 2018, mojawapo likiwa lile la KPL Top 8.

Ingawa ni jambo la kusikitisha sana, ambalo ni pigo kubwa kwa maendeleo ya soka ya humu nchini, ukweli ni kwamba tunakabiliwa na uchechefu mkubwa wa fedha,” alisema Oguda kwa kusisitiza kwamba huenda wakalazimika pia kufutilia mbali kipute cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 (KPL U-20). 

“Tungali katika mazungumzo ya kina na wadau mbalimbali na mashirika kadhaa kwa lengo la kutafuta fedha zitakazotuwezesha kuandaa kipute cha KPL U-20 mwakani.

Ni matumaini ya KPL kwamba fedha za kutosha zitapatikana kwa ajili ya kivumbi hicho,” akaongeza Oguda kwa kuonya kwamba watajipata katika ulazima wa kufuta michuano hiyo katika kalenda yao iwapo ufadhili wanaousaka hautapatikana kwa wakati. 

Mnamo Septemba 2017, vinara wa walifutilia mbali katika kalenda yao ya mwaka huu kivumbi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 16 (KPL Under-16) pamoja kuondoa katika bajeti yao gharama ya kulipia taa za kuendeshea mechi ambazo awali zilikuwa zimeratibiwa kusakatwa usiku. 

“Ilikuwa rahisi mno kuratibu mechi kadhaa za KPL hata usiku wakati tulipokuwa na wadhamini wetu wa SuperSport. Kwa sasa uchechefu wa fedha umetulazimu kuandaa michuano yote nyakati za mchana na alasiri,” akafafanua Oguda.