KRU: Ligi Kuu msimu huu itaanza Novemba 25

Na  GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, October 9  2017 at  17:23

Kwa Muhtasari

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limetangaza kuwa Ligi Kuu ya msimu 2017/2018 itang’oa nanga Novemba 25, 2017.

 

Katika taarifa yake, KRU imesema kuwa ratiba ya mechi itatolewa wakati wowote kutoka Oktoba 8.

Ligi Kuu almaarufu Kenya Cup inatarajiwa kushirikisha klabu 12 jinsi ilivyokuwa msimu uliopita. Klabu zilizosalia katika Ligi Kuu baada ya msimu 2016/2017 kukamilika ni KCB (mabingwa), Kabras Sugar, Homeboyz, Impala Saracens, Kenya Harlequins, Nakuru, Mwamba, Nondies, Strathmore Leos ya Chuo Kikuu cha Strathmore na Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mombasa na Kisii zimechukua nafasi za Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Western Bulls ambazo zilitemwa. Kisii inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kabisa. Mombasa inarejea kwenye Ligi Kuu baada ya kuwa nje misimu miwili. Ilitemwa baada ya msimu 2014/2015.