Kabras yatiwa kundi la kifo Christie Sevens

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, October 9  2017 at  17:44

Kwa Muhtasari

DROO ya duru ya Christie Sevens imetangazwa, huku raga za Kitaifa za wachezaji saba kila upande zikiratibiwa kurejea wikendi ya Oktoba 14-15, 2017 baada ya likizo ya wiki moja.

 

Kwenye droo ambayo Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) imetangaza Jumatatu, mabingwa wa Sepetuka Sevens Kabras Sugar wametiwa katika kundi A pamoja na Kenya Harlequins, Strathmore Leos na Mombasa.

Mabingwa wa Kabeberi Sevens Impala Saracens wako katika kundi B pamoja na Nakuru, Mean Machine na Kisii.

Viongozi wa mashindano haya ya duru sita Homeboyz, ambao walinyakua taji la Driftwood Sevens, wamekutanishwa na Western Bulls, Mwamba na Nondies katika kundi C.

Mabingwa wa Prinsloo Sevens KCB wako katika kundi la mwisho linalojumuisha Oilers, Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na Falcons ya Chuo Kikuu cha Daystar.

Homeboyz inaongoza jedwali kwa alama 68. Inafuatwa na Kabras (63), Impala (61), Oilers (58) nayo Nakuru inafunga klabu tano-bora kwa alama 56.

Kabras walilaza Homeboyz 22-5 katika fainali ya makala yaliyopita ya Christie Sevens uwanjani RFUEA jijini Nairobi.