http://www.swahilihub.com/image/view/-/5144226/medRes/2363037/-/i0eueg/-/kagere+pic.jpg

 

Kagere: Sijutii kujiunga na Simba

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, June 4  2019 at  10:37

 

Dar es Salaam. Mshambuliaji nyota wa Simba, Meddie Kagere amesema licha ya kuwindwa na klabu mbalimbali, lakini hana mpango wa kuondoka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Rwanda, alisema anataka kuitumikia Simba kwa muda marefu.

"Naipenda Simba nafurahia maisha ndani ya klabu hii, tangu nimejiunga nayo sijawahi kujuta, sina mpango wa kuondoka kuhamia timu nyingine kwa sasa," alisema Kagere.

Nyota huyo alisema ana mkataba na Simba na atakuwa tayari kuzungumza na uongozi wa klabu hiyo kumuongeza baada ya ule wa awali kumalizika.

Kagere aliibuka mfungaji bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika baada ya kupachika wavuni mabao 23 akifuatiwa na Heritier Makambo wa Yanga na Salim Aiyee wa Mwadui Shinyanga waliofunga 17 kila mmoja.

Kagere alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba waliopewa Sh24 milioni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana.

Makonda alitoa fedha hizo alizoahidi kuwapa wachezaji wa Simba waliofanya vizuri katika mashindano ya msimu huu.

"Ni motisha nzuri kwetu hii inaonyesha namna gani mchango wetu unathaminiwa, tutaendelea kupambana ili kuifanya Simba iendelee kuwa bingwa," alisema Kagere.

Kipa Aishi Manula alipata Sh10 milioni. Mchezaji wa Simba Queens, Mwanahamisi aliyepewa Sh 2 milioni na Ofisa Habari Haji Manara Sh3 milioni.

Wengine waliopewa fedha ni Erasto Nyoni, James Kotei, John  Bocco, Rashid Juma na Clatous Chama.