http://www.swahilihub.com/image/view/-/2592808/medRes/924238/-/nvrx7xz/-/sanchez.jpg

 

Kamwe simwachilii Sanchez, asema Wenger

Alexis Sanchez

Straika wa Arsenal Alexis Sanchez asherehekea bao la tatu katika mchuano wa Ligi Kuu Uingereza kati ya Arsenal na Stoke City uwanjani Emirates, London. Picha/AFP 

Na AFP

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  21:58

Kwa Muhtasari

ARSENE Wenger amesisitiza kwamba nyota Alexis Sanchez bado anapigania timu yake ya Arsenal kwa moyo wake wote licha ya kumuanzisha benchini katika mechi ya League Cup, Jumatano.

 

Wenger aliamua kumchezesha Sanchez dakika 25 za mwisho katika mechi ya nusu-fainali dhidi ya Chelsea iliyomalizika 0-0 uwanjani Stamford Bridge.

Uamuzi huu wa Wenger ulikuwa wa kijasiri hasa kwa sababu League Cup inaipa Arsenal nafasi ya pekee ya kushinda taji msimu huu.

Baadhi ya mashabiki wa Arsenal na wachanganuzi wanaamini Sanchez hajitolei asilimia 100 kwa sababu kandarasi yake inakaribia kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa amekataa kuiongeza, huku ripoti zikisema anachochea mgawanyiko kikosini.

Ingawa viongozi wa Ligi Kuu Manchester City wanataka sana kumsajili Sanchez baada ya kukosa kumnyakua mwezi Agosti, Wenger alidai kwamba Mchile huyu bado anajitolea kuchezea Arsenal licha ya kuonyesha msururu wa mchezo duni.

“Watu hawamjui Alexis Sanchez. Yeye ni mtu ambaye amejitolea kwa dhati kusakata kabumbu.

“Uliona alivyoteremka uwanjani? Alivyopasha misuli? Alionyesha yuko tayari kutandaza gozi.

“Anaweza kuleta tofauti katika kile kinachofanyika nje ya uwanja na pia kinachoendelea uwanjani.

“Tunaishi na ukweli na wala si nadharia za kiakili. Unapoingia uwanjani unacheza mpira na kujitolea asilimia 100. Hicho ndicho anachofanya kwa sasa,” alimtetea Sanchez.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba Wenger anaamini Sanchez bado anaweza kushawishiwa kusalia uwanjani Emirates.
“Ningependa asalie hapa kwa muda mrefu,” aliongeza.

“Sina tatizo akiongeza mkataba wake nasi katika kipindi hiki kifupi cha uhamisho cha Januari ama wakati wa kipindi kirefu cha uhamisho mwezi Juni.”

Winga wa Arsenal, Alex Iwobi alianza mechi badala ya Sanchez licha ya kukabiliwa na tishio la kupigwa faini kwa kuenda kujiburudisha saa chache kabla ya Nottingham Forest kubandua nje klabu yake katika Kombe la FA katika raundi ya tatu.

Alipoulizwa ikiwa kumuanzisha Iwobi badala ya Sanchez ilikuwa hatua iliyotuma ujumbe mbaya kuhusu nidhamu ya timu, Wenger alisema, “Kuadhibu mchezaji mmoja ni kitu tofauti kabisa na kuadhibu kikosi kizima.

“Niliona anaweza kusaidia timu kupata ushindi, lakini haimaanishi kwamba hawezi kuadhibiwa binafsi.”

Wenger, ambaye alifichua kwamba kiungo Jack Wilshere atakosa mechi ijayo mnamo Jumapili dhidi ya Bournemouth baada ya kuumia kifundo, alitazama mechi ya Chelsea kutoka kwa eneo la wanahabari akitumikia marufuku yake ya mechi tatu.

Wakati uo huo, kocha wa Chelsea, Antonio Conte, alisikitishwa na vijana wake kukosa kuona lango licha ya kutawala mchezo dhidi ya Arsenal.

Ilikuwa sare ya pili mfululizo ambayo Chelsea iliandikisha bila kupata bao. Kabla ya hapo, Chelsea iliumiza nyasi bure dhidi ya Norwich katika Kombe la FA. Conte sasa ameonya vijana wake kwamba wanastahili kujiimarisha kupata makali yao tena mbele ya goli.