http://www.swahilihub.com/image/view/-/5144256/medRes/2362997/-/dirfdf/-/kapombe+pic.jpg

 

Kapombe njia panda, aumia tena Stars

Na Thobias Sebastian, Mwananch

Imepakiwa - Tuesday, June 4  2019 at  10:51

 

Dar es Salaam. Beki nguli Shomari Kapombe ana hatihati ya kuongozana na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ katika safari ya kwenda Misri kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

Kapombe aliyeanza mazoezi ya viungo hivi karibuni akitokea katika maumivu ya muda mrefu, alipata jeraha katika eneo hilo wakati wa  mazoezi ya Taifa Stars.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka  Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema beki huyo yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa Simba na Taifa Stars.

“"Siku ya mwisho ya kambi hapa Dar es Salaam kocha ataamua kama Kapombe atakuwa sehemu ya kikosi kitakachokwenda Misri au vinginevyo,"alisema Ndimbo.

Pia John Bocco na Shabani Chilunda hawakuendelea na mazoezi baada ya kupata maumivu walipogongana katika harakati ya kuwania mpira.

Ingawa Bocco hakuendelea na mazoezi licha ya kuonekana fiti, Chilunda alifungwa bandeji katika kifundo cha mguu baada ya kuwekwa barafu kutuliza maumivu.

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini Juni 7 kwenda Misri kuweka kambi kabla kuanza fainali hizo Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

Tanzania imepangwa Kundi C na Kenya, Algeria na Senegal ambapo timu 24 za Afrika zinatarajiwa kushiriki fainali hizo.