Kenya Police yaipiga Eastern ya Misri magongo

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Tuesday, January 10  2017 at  20:59

Kwa Mukhtasari

MAAFISA wa polisi wa Kenya na Ghana walifunza klabu za Sharkia na Eastern kutoka Misri jinsi ya kucheza magongo katika Klabu Bingwa ya Afrika jijini Nairobi, Jumanne.

 

Kenya Police, ambayo ilifuzu kushiriki kipute hiki baada ya kumaliza Ligi Kuu ya Kenya katika nafasi ya pili mwaka 2015, iliduwaza mabingwa watetezi Eastern mabao 2-1 uwanjani City Park.

Wakenya hawa wanaonolewa na kocha Kenneth Kaunda walifungua kampeni yao kwa kupiga Wananchi ya Uganda 4-2 Januari 7.

Ushindi huu unaweka Kenya Police katika nafasi nzuri ya kufuzu kushiriki nusu-fainali. Vijana wa Kaunda watamenyana na Weatherhead ya Uganda mnamo Januari 11 na kumaliza mechi za kundi A dhidi ya Exchequers ya Ghana.

Mabingwa mara 23 wa Afrika, Sharkia, walizabwa 1-0 na Ghana Police katika mechi, ambayo Wamisri hawa walikuwa wamepigiwa upatu kuibuka na ushindi.

Katika mechi za wanawake zilizopigwa leo Jumanne, Orange ya Kenya, ambayo inatetea taji la wanawake, ilipepeta Weatherhead 9-0 nao mabingwa wa zamani Heartlands wakakabwa 2-2 na Ghana Police.