Kenya yakosa taji Delhi Half Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, November 19  2017 at  19:15

Kwa Muhtasari

KENYA imemaliza mbio za Delhi Half Marathon nchini India bila taji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2008.

 

Katika makala ya mwaka 2017 yaliyoandaliwa mapema Novemba 19, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 10,000 Almaz Ayana aliongoza Waethiopia wenzake Ababel Yeshaneh na Netsanet Guideta kunyakua nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanawake.

Ayana alikuwa anashariki mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza kabisa. Alikamilisha umbali huo kwa saa 1:09:11, sekunde tisa mbele ya Yeshaneh na sekunde 13 mbele ya Guideta.

Waethiopia Berhanu Legese na Andamlak Belihu walinyakua nafasi mbili za kwanza katika kitengo cha wanaume, huku Muamerika Leonard Korir, ambaye ni mzawa wa Kenya, akiridhika katika nafasi ya tatu. Ni taji la pili la Berhanu katika Delhi Half Marathon baada ya kushinda mwaka 2015.

Kabla ya kuambulia pakavu mwaka 2017, Kenya ilikuwa imeshinda taji la Delhi Half Marathon kupitia Mary Keitany (2009), Geoffrey Mutai (2010), Lucy Kabuu (2011), Edwin Kipyego (2012), Florence Kiplagat (2013 na 2014), Cynthia Limo (2015) na Eliud Kipchoge (2016).

Wakiambiaji 35,000, akiwemo bingwa wa mbio za kilomita 42 za wanaume duniani Mkenya Geoffrey Kirui, walishiriki makala ya 13.   

 

Matokeo (Novemba 19, 2017):

Wanaume

Berhanu Legese (Ethiopia) dakika 59:46

Andamlak Belihu (Ethiopia) 59:51

Leonard Korir (Marekani) 59:51

 

Wanawake

Almaz Ayana (Ethiopia) saa 1:07:11

Ababel Yeshaneh (Ethiopia) 1:07:20

Netsanet Guideta (Ethiopia) 1:07:25