Kenya yasalia pale pale katika viwango vipya vya raga

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, July 17   2017 at  16:44

Kwa Mukhtasari

UGANDA inaendelea kukwea jedwali la viwango bora vya raga duniani, huku Kenya na Namibia zilisalia katika nafasi za 26 na 21 baada ya mechi za raundi ya nne za Africa Gold Cup zilizopigwa Julai 15.

 

Waganda, ambao waliruka kutoka 45 hadi 40 walipokaba Kenya 33-33 Juni 24 na kuimarika tena hadi 38 walipozaba Senegal 17-16 Julai 8, sasa wanashikilia nafasi ya 36 baada ya kupepeta Tunisia 78-17 jijini Kampala, Julai 15.

Katika viwango vipya vilivyotangazwa Jumatatu na Shirikisho la Raga duniani (World Rugby), New Zealand, Uingereza, Ireland, Australia, Afrika Kusini, Scotland, Wales, Ufaransa, Argentina na Fiji zinafuatana kutoka nafasi ya kwanza hadi 10, mtawalia. Hakuna mabadiliko katika mduara huo.  Japan, Georgia, Tonga na Italia pia zimesalia katika nafasi za 11, 12, 13 na 14, huku Romania ikirukia nambari 15 na kusukuma Samoa nafasi moja chini hadi 16 duniani.

Katika msimamo wa Afrika, Afrika Kusini ni ya kwanza ikifuatwa na Namibia (21 duniani), Kenya (26), Zimbabwe (35) nayo Uganda inapumua nyuma ya Zimbabwe katika nafasi ya 36.

Moldova na Ukraine kutoka bara Ulaya ziliathiriwa na ushindi wa Uganda. Zimeteremka nafasi moja chini na kutua katika nafasi za 37 na 38 duniani, mtawalia.

Barani Afrika, Morocco imesalia katika nafasi ya 42 nayo Madagascar imepaa nafasi moja hadi 48 duniani. Guyana kutoka Amerika Kusini imeimarika kutoka 50 hadi 49 nayo Senegal inafunga 50-bora baada ya kuruka juu nafasi moja. Tunisia, ambayo imepigwa 53-7 na Namibia, 100-10 na Kenya na Uganda, imeshuka nafasi tatu na sasa inashikilia nambari 51 duniani. Hakuna mabadiliko mengine katika viwango hivi bora vya mataifa 103.

Kombe la Afrika (Gold Cup) litaendelea Julai 22 ambapo Kenya itamenyana na Zimbabwe mjini Bulawayo nayo Uganda ikabane koo na Namibia jijini Kampala.

Kwingineko, Kenya Simbas ya kocha Jerome Paarwater imepangiwa kurejelea mazoezi yake jijini Nairobi, Jumatatu jioni. Inajiandaa kwa safari ya Afrika ya Kusini itakayoanzia Zimbabwe na kukamilika dhidi ya Namibia hapo Julai 29.