http://www.swahilihub.com/image/view/-/5155728/medRes/1834928/-/t40ac9/-/ninje+pic.png

 

Kilichomng’oa Ninje TFF hiki hapa

Na Thobias Sebastian na Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, June 13  2019 at  12:37

 

Dar es Salaam. Matokeo mabaya iliyopata timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ yamechangia kwa kiasi kikubwa kumngoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ammy Ninje.

Pia matokeo yasiyoridhisha iliyopata timu ya Taifa ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ katika michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2017, yamechangia Ninje kuondolewa katika wadhifa wake.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alidai Ninje ameondolewa katika nafasi hiyo kutokana na sababu za kifamilia.

Karia alisema mbali na Ninje, shirikisho hilo limeondoa aliyekuwa kocha mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo aliyeiongoza katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Aprili, mwaka huu.

Katika fainali za Afcon, Serengeti Boys ilifungwa mechi zote tatu, ilichapwa mabao 4-2 dhidi ya Angola, ilichapwa 3-0 na Uganda kabla ya kunyukwa 5-4 na Nigeria.

Ninje akiwa Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars katika Kombe la Chalenji iliyochezwa Kenya, Desemba 2017, timu hiyo ilitoka suluhu dhidi ya Libya, ilichapwa 1-0 na Kenya, ililala 2-1 ilipovaana na Rwanda kabla ya kucharazwa 2-1 na Zanzibar katika mechi ya robo fainali.

Matokeo hayo yasiyoridhisha huenda yakawa ni sababu ya kigogo huyo kupoteza sifa ya kuwa mkurugenzi wa ufundi wa TFF.

"Atakwenda kusoma na kuangalia famialia yake kwa ukaribu Uingereza na kwasababu hiyo tumekubaliana kuachana naye katika nafasi hiyo.

"Hatuna shida yoyote kati yetu, tumeachana naye kwa amani kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanyia shirikisho. Nina imani tutapata mbadala sahihi ambaye atakuja kuziba nafasi," alisema Karia.

Kauli ya Ninje

Ninje alisema ameomba kuondoka katika nafasi hiyo ili kupata nafasi ya kwenda Uingereza kukaa karibu na familia yake.

"Nimeondoka katika nafasi hii  na sina tatizo na mtu, maneno ambayo yanaongelewa si ya kweli. Kwa muda niliokuwa TFF, nimefanya kazi nyingi na nimeacha alama ikiwemo Taifa Stars kufuzu AFCON,”alisema Ninje.

Kayuni atajwa

Kocha wa Prisons Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Ninje amedumu katika nafasi hiyo kwa muda mfupi, lakini ametoa rai kwa TFF kutafuta mtu sahihi wa kuziba nafasi hiyo.

"Kama atapatikana mbadala wake basi naomba apatikane kama Sunday Kayuni na afanye mambo ya msingi kama ambavyo alikuwa anafanya kiongozi huyo ambaye alikuwa sahihi katika nafasi hiyo," alisema Rishard.

Kocha wa zamani wa Yanga Kenny Mwaisabula alisema kama angepata nafasi ya kumtafuta mbadala wa Ninje angemchagua Kayuni aliyedai ana sifa za kushika wadhifa huo.

"Kama wameamua kumuacha Ninje kutokana na sababu walizotaja wao nadhani watakuwa sahihi, lakini katika kipindi kama hiki timu ya Taifa ipo katika mashindano muhimu wangesubiri yamalizike,"alisema Mwaisabula.

Kayuni amewahi kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF enzi ya utawala wa waliokuwa rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga na Jamal Malinzi.