Kipingu, Pazi watoa neno Afcon

Na IMANI MAKONGORO, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  14:40

Kwa Muhtasari

Kipa nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Iddi Pazi amesema ana hofu kama mashindano ya vijana chini ya miaka 17 ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini yatakuwa ya kiwango bora.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

ZIKIWA zimebaki siku 74 kabla ya kuanza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (Afcon), baadhi ya wadau wameonyesha wasiwasi kama yatafanyika kwa kiwango bora kama ilivyotarajiwa na wengi.

Tanzania inayowakilishwa na Serengeti Boys, itakuwa mwenyeji wa fainali hizo zilizopangwa kuanza Aprili 14 hadi 28, mwaka huu zikishirikisha nchi nane za Afrika.

Mwenyekiti wa zamani Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu, Iddi Kipingu alisema maandalizi ya nchi hayaendani na ukubwa wa mashindano.

Kipingu alisema zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika fainali hizo, hakuna hamasa inayoitangaza Tanzania kama mwenyeji wa mashindano hayo.

"Ingawa wanatarajia kuweka kambi nje, lakini kinachofanyika katika maandalizi yao bado, walipaswa kucheza mechi za kirafiki hata na timu zetu za vijana mara nyingi iwezekanavyo wakati wakisubiri kuondoka, lakini hakuna kitu kama hicho," alisema Kipingu.

Alisema maandalizi yanayofanywa ni sawa na Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikiahidiwa fedha na motisha kwa wachezaji zinapokaribia kucheza mechi baina yao au za mashindano.

"Wasiwasi wangu timu yetu ya vijana isije kukutana na jambo kama hilo, badala ya kuwasaidia na kuwapa morali, inaweza kuwapa taharuki na kujikuta wanashindwa kufanya vizuri, lakini wakizoeshwa mapema watachukulia mashindano ya kawaida," alisema Kipingu.

Kipa nyota wa zamani wa Simba na Taifa, ‘Taifa Stars’, Idd Pazi alisema anashangaa kuona ukimya na hakuna taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya fainali hizo wakati Tanzania ni mwenyeji wa mashindano.

"Nchi nyingine inapokuwa mwenyeji wa mashindano tunaona namna wanavyohamasishana, mfano Olimpiki ya mwaka 2020, Wajapan wanahamasishana kweli, huu ulikuwa wakati wa Tanzania kuonyesha hamasa hiyo.

"Hata kwenye vyombo vya habari, kungekuwa na matangazo ya Afcon ya vijana yanapita, yanaielezea Tanzania na maandalizi ya michezo hiyo kila baada ya muda fulani, lakini tuko kimya," alisema Pazi.

Mazoezi ya muda wa saa nne kila siku

Hata hivyo, Serengeti Boys inaendelea na mazoezi Uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park, Kidongo Chekundu, Dar es Salaam, chini ya kocha Oscar Mirambo, aliyesema yanafanyika kwa saa nne kila siku.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ammy Ninje alipoulizwa kuhusu maandalizi ya Serengeti Boys kujiandaa na fainali hizo alisema atafutwe Ijumaa wiki ijayo.

"Siko kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo, lakini Ijumaa nitakuwa katika mazingira mazuri ya kuzungumzia ushiriki wetu na maandalizi ya timu kwa ujumla," alisema Ninje.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini, Yusuph Singo alisema maandalizi yako katika hatua nzuri ikiwamo ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo.

"Watu wanaweza kuona kama tuko kimya, lakini mambo yanakwenda vizuri, ikiwamo kurekebisha miundombinu ya viwanja, baadhi ya barabara za kuingia na kutoka kwenye viwanja vitakavyotumika, hoteli ambazo timu zitafikia na mambo mengine.

"Vikao vinaendelea, bajeti yetu ni kubwa mno, lakini tunaamini kila kitu kitakuwa sawa," alisema Singo.