http://www.swahilihub.com/image/view/-/5022684/medRes/2177521/-/4s31qmz/-/klabu+pic.jpg

 

Klabu Ligi Kuu Bara zaingia matatani

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao 

Na Oliver Albert, Mwananchi oalbert@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Wednesday, March 13  2019 at  10:03

 

Dar es Salaam. Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zimelaumiwa kwa  utovu wa nidhamu, baada ya idadi kubwa ya makatibu wake wakuu kukacha semina iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema kitendo cha idadi kubwa ya klabu hizo kutuma wawakilishi katika semina ya makatibu wakuu hakikubaliki.

"Nashangaa klabu zimeleta watu wengine ambao hawafanyi kazi za kila siku za kiutendaji za klabu. Nia na madhumuni ya semina ilikuwa kuwajengea uwezo makatibu wakuu.

Katibu Mkuu huyo alisema TFF imesikitishwa na kitendo hicho alichodai kinarudisha nyuma maendeleo ya soka nchini.

Akizungumzia jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mguto alisema viongozi wa klabu wamekuwa wakidharau semina za TFF zinazoandaliwa kwa manufaa yao.

"Inasikitisha kuona mahudhurio hafifu, klabu nyingi zimetuma wawakilishi wengi hawafahamu umuhimu wao kama makatibu na nguvu yao katika klabu.

Katibu Mkuu wa JKT Tanzania Abdul Nyumba alisema:”Semina kama hizi ni muhimu zinatujengea uwezo wa kusimamia mambo mbalimbali kwa ufanisi”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga alisema semina hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya klabu na soka kwa jumla.

Emmanuel Kimbe ambaye ni Katibu Mkuu wa Mbeya City, alidai  alishindwa kuhudhuria  kutokana na kubanwa na majukumu ya kazi.

“Sikufanya makusudi kutohudhuria majukumu mengine ya kazi yalinibana, lakini semina hizo ni muhimu kwa maendeleo ya klabu na soka,”alisema Kimbe.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Kanali Mstaafu Idd Kipingu alisema ingawa semina ni muhimu lakini  huenda kuna  sababu inayochangia idadi kubwa ya makatibu kukacha.