Klabu ya Olunga yajikwaa dhidi ya Bilbao

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, September 11  2017 at  12:19

Kwa Mukhtasari

KLABU ya Girona anayochezea Mkenya Michael Olunga ilijikwaa katika mechi yake ya tatu ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kulimwa 2-0 na Athletic Bilbao ugenini, Jumapili.

 

Mshambuliaji Olunga, ambaye alijiunga na Girona mnamo Septemba 1, 2017 kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Guizhou Zhicheng ya Uchina, alikuwa kwenye benchi.

Mvamizi Iker Muniain aliipa Bilbao bao la ufunguzi dakika ya 25 baada ya kupata krosi safi iliyochotwa na Inaki Williams hadi ndani ya kisanduku kutoka pembeni kulia.

Inaki pia alimega pasi murwa iliyomaliziwa kwa ustadi na Aritz Aduriz katika dakika ya 53. Refa alitoa kadi 10 za njano katika mechi hii iliyopigiwa uwanjani San Mames. 

Girona itamenyana na Sevilla katika mechi yake ijayo hapo Septemba 17 kabla ya kukabiliana na Barcelona inayojivunia nyota kama Lionel Messi na Luis Suarez mnamo Septemba 23. Italimana na mabingwa watetezi Real Madrid mnamo Oktoba 29. 

Barcelona inaongoza ligi hii ya klabu 20 kwa pointi tisa baada ya kushinda mechi zake tatu za kwanza.

Sevilla inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi saba nayo Madrid ni ya saba kwa alama tano. Girona inashikilia nafasi ya 11 kwa pointi nne ambazo ilipata kutoka kwa sare ya 2-2 dhidi ya Atletico Madrid (Agosti 19) na ushindi wa 1-0 dhidi ya Malaga (Agosti 26).