Klopp akataa kuipa ubingwa Liverpool

Jurgen Klopp 

Imepakiwa - Friday, December 28  2018 at  10:44

Kwa Muhtasari

Alisema timu nyingi bado zina nafasi ya kutwaa ubingwa

 

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema watu waendelee kusubiri hadi mechi za mwisho kumuona bingwa wa Ligi Kuu England kuliko kusema hivi sasa Liverpool ndiye bingwa.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya kuichapa Newcastle mabao 4-0, Klopp alisema timu nyingi bado zina nafasi ya kutwaa ubingwa ikiwemo Arsenal, Tottenham, Chelsea, Man City na hata Manchester United.

Hata hivyo, kwa mchezo wa juzi, vijana wa Jurgen Klopp sasa wako mbele kwa pointi sita baada ya mabao ya; Dejan Lovren, Mohamed Salah, Xherdan Shaqiri na Fabinho.

Manchester City ililala tena kwa mabao 2-1 dhidi ya Leicester mpambano uliofanyika kwenye Uwanja wa King Power ikiwa ni mchezo wake wa tatu kupoteza.

Bernardo Silva aliifungia Man City bao la kuongoza kabla ya Marc Albrighton kusawazisha lakini Ricardo Pereira akamaliza mchezo dakika ya 81 kwa kuipa pointi muhimu Foxes.

Tottenham nayo imepanda hadi nafasi ya pili ikiishusha Manchester City ikiwa na pointi sita pungufu kwa vinara Liverpool, baada ya kuikandamiza Bournemouth 5-0.

Kocha mpya wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer aliendelea kung’ara baada ya kuirarua Huddersfield 3-1 huku Paul Pogba akitupia mara mbili. Everton ilifunga mabao matatu ndani ya dakika 22 kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Burnley, wakati

Crystal Palace ilitoka suluhu na Cardiff. Fulham iliendelea kukalia mkia baada ya sare ya 1-1 na Wolves.

Nayo Brighton ilitoka nyuma na kusawazisha bao dhidi ya Arsenal, kupitia kwa Jurgen Locadia akifuta mabao ya Pierre-Emerick Aubameyang. Chelsea iliipiga kumbo Arsenal kwenye nafasi ya nne kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Watford huku Eden Hazardakitupia mabao yote mawili.

Mshambuliaji huyo wa Ubelgiji alifunga bao la 100 na kuwa mchezaji wa 10 kufanya hivyo katika historia ya klabu.