http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842402/medRes/2131454/-/gdv3hyz/-/klop.jpg

 

Klopp ang’aka kipigo Ulaya

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  12:44

Kwa Muhtasari

Tulianza mchezo vizuri lakini tulijimaliza kwa kushindwa kufunga na kupoteza

 

Belgrade, Serbia. Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp, amesema hafahamu nini kimewapata wachezaji wake katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Klopp aliyeiongoza Liverpool kucheza fainali msimu uliopita bila kupoteza, juzi aliduwazwa na Red Star Belgrade ya Serbia kwa kulala mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano.

Alisema timu yake haikutarajia kipigo hicho kwa kuwa katika mechezo wa kwanza iliifunga Red Star mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Anfield, mwezi uliopita.

Klopp alisema hata mchezo wao dhidi ya PSG hawakucheza vizuri kulinganisha na kile walichofanya msimu uliopita.

“Tulikuja tukiwa na matumaini ya ushindi, tulianza mchezo vizuri lakini tulijimaliza kwa kushindwa kufunga na kupoteza,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Klopp alisema wachezaji walitawala mchezo huo, lakini walikuwa na tatizo la umaliziaji ambalo liliwapa wakati mgumu kukomboa mabao waliyofungwa mapema na Milan Pavkov dakika za 22 na 29.

Kocha huyo alikiri kuwa baada ya kufungwa mabao hayo walipoteza umakini na kucheza kwa hofu licha ya kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa.

“Tulitawala mchezo kipindi kirefu, lakini wenyeji hawakutupa nafasi ya kufunga jambo lililoongeza presha, nawapongeza kwa hilo, kuna kitu tunapaswa kujifunza,” alisema kocha huyo.

Klopp alidai makosa waliyofanya katika mchezo huo hayatajirudia katika mechi zijazo za mashindano mbalimbali.

Alisema hawatapoteza muda kujadili matokeo ya mchezo huo na watatafakari nini cha kufanya ili kupata ushindi katika mechi zijazo ambapo Jumapili wiki hii wataikaribisha Fulham katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo alisema watasahihisha makosa lengo ni kupata matokeo mazuri.