http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119558/medRes/2346497/-/135ep3uz/-/kocha+pic.jpg

 

Kocha Alliance ataka pointi tatu

Na Saddam Sadick, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  11:28

 

Mwanza. Kocha wa Alliance, Malale Hamsini amesema anataka pointi tatu katika mchezo dhidi ya Stand United ambazo zitaibakiza timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Kauli ya Hamsini imekuja muda mfupi, baada ya timu hiyo kuigagadua Biashara United mabao 2-1. Alliance ipo nafasi ya 10 ikiwa na pointi 44 na imebakiza mechi mbili kumaliza ligi.

Endapo Alliance itashinda Jumatano wiki ijayo dhidi ya Stand United, itajiweka katika mazingira mazuri ya kubaki kwenye mashindano hayo.

Hamsini alisema ingawa ana kibarua kigumu katika vita ya kujinasua na janga la kushuka daraja, lakini matokeo hayo yameshusha presha kwa timu hiyo.

Kocha huyo amewapongeza wachezaji wanavyopambana kuinusuru timu na janga hilo, hivyo mechi zinazofuata bado zina umuhimu kwao kumaliza ligi katika nafasi salama.

“Bado tuna kazi ngumu ya kupambana katika mechi zilizobaki. Nia na malengo yetu ni kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu msimu ujao, kwahiyo tunaenda kujipanga dhidi ya Stand United,”alisema Hamsini.

Kocha huyo aliongeza ligi msimu huu imekuwa na ushindani mkali kutokana na kwamba hakuna aliyejihakikishia ubingwa,huku timu nyingi zikihaha kukwepa kushuka daraja.

“Angalia msimamo timu inayopoteza mchezo mmoja inashuka nafasi za chini, kwahiyo utagundua hali ni ngumu lakini hata bingwa hajajulikana lazima Alliance tuzidi kupambana,”alisema kocha huyo.