Kocha Tietjens kupata mshahara mnono kuliko rais na waziri mkuu

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Sunday, October 23  2016 at  14:09

Kwa Muhtasari

KOCHA Gordon Tietjens, ambaye Kenya ilitaka huduma zake, atakula mshahara zaidi ya Rais na Waziri Mkuu wa Samoa kuinoa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya nchi hiyo atakapochukua usukani Januari 1 mwaka 2017.

 

Tietjens alipuuza Shujaa na kujiunga na wanavisiwa hao Oktoba 14 mwaka 2016.

Kulingana na tovuti ya stuff.co.nz, raia huyu wa New Zealand atapokea zaidi ya Sh8 milioni kama mshahara wake wa kila mwaka (karibu Sh692, 000 kila mwezi).

Rais wa Samoa, Tui Atua Tupua Tamasese Tupuola Tufuga Efi anapokea Sh8.3 milioni kila mwaka naye Waziri Mkuu Tuilaepa Malielegaoi anatia kibindoni Sh7.9 milioni kila mwaka.

Tietjens, 60, atakosa duru mbili za ufunguzi za Raga za Dunia zitakazoandaliwa katika miji ya Dubai (Milki za Kiarabu) na Cape Town (Afrika Kusini) mwezi Desemba mwaka 2016.

Duru ya Dubai itapigwa Desemba 2-3, ambapo Samoa itakutana na New Zealand, Uingereza na Urusi katika kundi C.