Kocha wa Western Stima awataka madifenda kujiamini

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:21

Kwa Muhtasari

KOCHA mpya wa Western Stima, Richard Makumbi amewataka wachezaji wake kujiamini baada ya kuhusisha matokeo duni ambayo yamesajiliwa na kikosi hicho hadi kufikia sasa msimu huu na kubabaika kwa walinzi.

 

Stima ambayo ilitamba sana katika msimu wa 2016 na kutinga mduara wa nane-bora, imesajili msururu wa matokeo duni katika kampeni za 2017 na kipo ipo katika hatari ya kuteremshwa ngazi katika kivumbi cha Ligi Kuu mwishoni mwa msimu huu.

Hadi kufikia sasa, Stima wanashikilia nafasi ya 16 kwa alama 31 sawa na mabingwa wa KPL 2008, Mathare United.
Makumbi amesema kwamba endapo mtazamo hasi haungetawala vijana wake, wangefanya vyema zaidi katika kampeni za msimu huu. 

“Licha ya kwamba wengi wa wachezaji ni kiwango cha kimataifa, baadhi yao wanakosa kujiamini. Ni lazima wakubali kwamba wana vipaji tele vinavyofaa kuchochewa hata zaidi na tajriba ya miaka mingi.

Soka ndiyo taaluma yao na kimsingi ni lazima wajikakamue kwa sababu hapa ndipo wanapovuna ujira wao", alisema kocha huyo aliyemrithi Henry Omino mnamo Septemba 2017.