http://www.swahilihub.com/image/view/-/4920792/medRes/2180932/-/ywsj18z/-/mo.jpg

 

Kufuru mpya ya MO Dewji Simba

Mohammed ‘Mo’ 

Na THOBIAS SEBASTIAN

Imepakiwa - Friday, January 4  2019 at  10:07

Kwa Muhtasari

Ametenga Sh 1 bilioni kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika

 

BILIONEA wa Simba, Mohammed ‘Mo’ hataki utani kabisa, baada ya kubainika ametenga Sh 1 bilioni kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa yuko mbioni kuiletea basi kali la aina yake kwa ajili ya timu.

Imedokezwa fedha hizo zilizotengwa na Mo zilianza kutumika katika mechi nne za awali na kilichobaki ni maalumu kwa ajili kuhakikisha Simba inapenya robo fainali Afrika.

Simba inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu walipocheza hatua hiyo mara ya kwanza 2003 na kwa sasa imepangwa Kundi D na Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DR Congo.

Chanzo makini toka ndani ya Simba kilifichua kuwa katika mechi nne za awali walitumia zaidi ya Sh 150 milioni tofauti na bajeti waliyojiwekea ya Sh 100 milioni kwa nje na Sh 30 milioni kwa mechi za ndani.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mulamu Nghambi alisema licha ya kutenga bajeti ndefu, lakini hataweka hadharani.

Alisema bajeti ya mashindano yote kwa ujumla hadi timu itakapoishia ni ngumu na malengo ya Simba ni kufika mbali zaidi na kila hatua watakuwa na bajeti yake kulingana na mechi na mpinzani husika.

“Katika mechi mbili za Mbabane na Nkana tulitumia Sh 150 milioni kama posho, kambi, usafiri, malazi na mambo mengine ambayo yanakuwa sawa na Sh 300 milioni hizo ni zile mbili za ugenini tu.

“Baada ya hapo tukacheza mechi mbili za nyumbani ambazo tulitumia si chini ya Sh 30 milioni kwa maandalizi na mambo mengine ya msingi kwa wachezaji na jumla ya mechi mbili ni kama Sh 60 milioni.

“Hatua ya makundi tutacheza mechi tatu ugenini ambazo kila moja gharama ya awali tumeweka Sh 150 milioni ili kuhakikisha tunafanya vizuri, lakini inaweza kubadilika kwa kuangalia na mazingira ikiwemo umbali wa safari. Kwa maana hiyo mechi tatu za ugenini ambazo tutacheza msimu huu tutatumia zaidi ya Sh 450 milioni,” alisema.

MO KULETA BASI

Katika hatua nyingine mabosi hao wa Simba wakiwa katika maandalizi ya kuhakikisha timu inafanya vizuri Afrika, wameendelea kufanya mambo makubwa ili kuonesha ukubwa wa timu hiyo, ikiwamo taarifa za kuletwa kwa basi la kisasa.

Inaelezwa licha ya Simba ya MO kuendelea kujenga uwanja wao wa mazoezi uliopo Bunju ambao, upo katika hatua nzuri kwa eneo la kuchezea, lakini pia kuna uwezekano wa kushushua basi la maana na la kisasa kama lile la Azam FC.

Basi la Azam lina kila kitu kama ndege vile, jambo ambalo limeifanya klabu hiyo kuwa mfano wa kuigwa, lakini inaelezwa Simba wanajipanga kujibu mapigo. Kwa sasa Simba inatumia basi ambalo ni sehemu ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kama ilivyo kwa Yanga.

Hata hivyo, Nghambi alipoulizwa alisema akili zao kwa sasa ni kukamilisha uwanja huo ili kupata eneo la kuchezea kwa kufanya mazoezi na kupunguza gharama za kukodisha viwanja wakati wa mazoezi.

“Sidhani kama kuna jambo lingine tutalofanya kwa wakati huu zaidi ya kuhakikisha tumaliza kwanza ujenzi wa uwanja kule Bunju ambao upo kwenye hatua nzuri. Kisha mambo ya usafiri ambao pia ni muhimu sana kwa timu yatafuata,” alisema Nghambi.