MAKALA: Ni Al Ahly na Casablanca fainali ya CAF 2017

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, October 24  2017 at  21:12

Kwa Muhtasari

MAGWIJI wa soka kutoka Misri, Al Ahly walifuzu kwa fainali ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu huu baada ya kuwakomoa Etoile Sahel ya Tunisia 6-2 jijini Alexandria mnamo Oktoba 22, 2017.

 

Awali, kikosi hicho ambacho kwa sasa kitavaana na Wydad Casablanca katika fainali ya mechi za mikondo miwili ilikuwa imewakandamizwa na Etoile kwa mabao 2-1 jijini Tunis katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Mechi ya awamu ya kwanza katika fainali ya mwaka huu wa 2018 itatandazwa nchini Misri mnamo Oktoba 28, 2017.

Tangu kuanzishwa kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika mnamo 1964, ni klabu tisa pekee ambazo zimewahi kufanikiwa kuvuna jumla ya mabao matano kutokana na mchuano mmoja wa nusu-fainali. Hivyo, ushindi wa Al Ahly uliwaweka katika mabuku ya historia ya kipute hicho.

Conakry II na Hafia kutoka Guinea, Mufulira Wanderers ya  Zambia, Bilima kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo), Shooting Stars ya Nigeria, Mouloudia Oran kutoka Algeria na wafalme wa soka nchini Ivory Coast, ASEC Mimosas ndizo klabu za pekee ambazo zimewahi kufikia ufanisi wa kiwango hicho.

TP Mazembe kutoka DR Congo na Wydad walifikia rekodi za klabu hizo tangu kivumbi hicho kibadilishwe jina na kuitwa CAF Champions League mnamo 1997.

Kabla ya kuzititiga nyavu za Etoile mara sita, mabao mengi zaidi yaliyowahi kufungwa na Ahly ni manne katika mechi ya nusu-fainali ya CAF iliyowakutanisha na Enugu Rangers ya Nigeria jijini Alexandria mnamo 1982.

Al Ahly walinogesha fainali ya CAF kwa mara ya mwisho mnamo 2013 ambapo walifanikiwa kuwabamiza Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-1, nyota mstaafu na nguli Mohames Abou Trika akiwa miongoni mwa masogora waliocheka na nyavu za Pirates.

Al Ahly walitawazwa mabingwa wa CAF Champions League kwa mara ya kwanza mnamo 1982 kabla ya kutia kapuni mataji mengine mawili ya kivumbi hicho kwa miaka miwili kwa mpigo.

Mbali na kufuzu kumenyana na Pachuca ya Mexico katika kipute cha kuwania Kombe la Dunia kitakachoandaliwa katika Nchi za Milki za Kiarabu (UAE) mnamo Desemba 2017,  mshindi wa taji la CAF Champions League mwaka huu pia atatawazwa kima cha Sh250 milioni.