MAKALA: Siasa za Catalonia zinavyotishia ndoto ya Olunga

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:28

Kwa Muhtasari

ALIYEKUWA mfumaji wa Gor Mahia ambaye kwa sasa ni mvamizi matata kambini Harambee Stars, Michael Olunga anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kubanduka Girona FC kufuatia hatua ya hivi majuzi ya Catalonia kutaka kujiondoa kutoka Uhispania na kuwa taifa huru.

 

Gazeti la Turkish Football limekiri kwamba vinara wa Osmanlispor wameanzisha mazungumzo na waajiri wa Olunga katika juhudi za kumshawishi nyota huyo kubanduka rasmi kambini mwa Guizhou Hengfeng Zhicheng ambao walimsajili kwa kima cha Sh480 milioni kutoka Djurgardens IF ya Uswidi mwanzoni mwa mwaka huu.

Kabla ya kuhamia Zhicheng kwa mkataba wa miaka minne, huduma za Olunga zilikuwa zikiwaniwa pia na CSKA Moscow (Urusi), Galatasaray (Uturuki), Olympique Lyon (Ufaransa) na Real Betis (Uhispania). 

Licha ya uhamisho wa Olunga kutoka Uswidi hadi China kupigiwa upatu kuwa chanzo cha kuimarika zaidi kwa kiwango cha ubora wa usogora wake, Zhicheng ambao walipandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya China mwanzoni mwa msimu jana, walifikia uamuzi wa kumwondoa sogora huyo katika mipango yao ya baadaye na kumtuma kwa mkopo wa mwaka mmoja kambini mwa Girona FC inayoshiriki kipute cha La Liga.

Kwa pamoja na Aly Ghazal ambaye ni kiungo mzawa wa Misri, Olunga anayetia mfukoni kima cha Sh12 milioni kwa mwezi aliondolewa katika orodha ya wachezaji watakaowajibikia kikosi cha kwanza cha Zhicheng msimu huu na hivyo kupangiwa katika kikosi cha akiba ambacho aghalabu huwajumuisha chipukizi wasiojivunia tajriba pevu katika taaluma ya usakataji kabumbu. 

Hatua hiyo ambayo inayumbisha pakubwa mustakabali wa Olunga imemweka Ghazal katika ulazima wa kukatiza ghafla uhusiano wake na Zhicheng na nyota huyo tayari amerejea Misri kwa matumaini ya kupata hifadhi mpya katika kikosi kingine.

Kwa pamoja, Ghazal na Olunga waliingia katika sajili rasmi ya Zhicheng mwanzoni mwa msimu jana baada ya kubanduka katika vikosi vilivyowapa hifadhi nchini Ureno na Uswidi mtawalia.

Kuteremshwa ngazi kwa Ghazal na Olunga ni hatua iliyochochewa na maamuzi ya Zhicheng kujitwalia huduma za nyota wawili matata wazawa wa Uhispania, Mario Suarez na Ruben Castro ambao waliagana rasmi na klabu za Watford (Uingereza) na Real Betis (Uhispania) mtawalia.

Ujio wa wawili hao uliwaweka Zhicheng katika ulazima wa kuondoa wachezaji wawili katika orodha ya kikosi chao cha kwanza kwa mujibu wa sheria zinazodhibiti soka inayopigwa na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya China (Chinese Super League). 

Girona ambayo iliasisiwa mnamo Julai 23, 1930, ilipandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu hupiga mechi zake za nyumbani katika uwanja wa Estadi Montilivi ambao una uwezo wa kubeba jumla ya mashabiki 13,500 pekee.

Kabla ya kutua ughaibuni, Olunga Olunga alichezea Tusker katika msimu wa 2013, Thika United (2014) na Gor Mahia (2015) kwa mkopo kutoka Liberty Sports Academy. 

Akiwa Gor, Olunga alimaliza wa pili katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya KPL. Olunga ni Mkenya wa tatu baada ya McDonald Mariga na mzawa wa Uhispania, Ismael Athuman Gonzalez kucheza soka ya kulipwa nchini Uhispania. 

Mariga alichezea Real Sociedad mnamo 2013 kwa mkopo kutoka Inter Milan ya Italia huku Las Palmas ikimpa hifadhi Gonzalez.