MAKALA: Teknolojia ya VAR itakavyoimarisha CHAN 2018

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:36

Kwa Muhtasari

SHIRIKISHO la Soka la Afrika (CAF) limethibitisha kwamba marefa watakaosimamia michuano ya fainali za CHAN 2018 nchini Morocco watasaidiwa na teknolojia ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya kipute hicho itatumia video maalum almaarufu VAR.

 

Licha ya VAR kukumbatiwa pakubwa katika Ligi Kuu za Uingereza, Ufaransa, Italia na Ujerumani, suala la kujumuishwa kwa teknolojia hiyo katika Ligi ya Uhispania (La Liga) lilitupiliwa mbali miaka miwili iliyopita kutokana na wingi wa gharama ya kuifanikisha hatua hiyo.

Iliwajuzu Barcelona kukabiliana vilivyo na pigo la kunyimwa bao la ufunguzi baada ya mpira ulioelekezwa na Lionel Messi langoni pa Valencia kumzidi maarifa kipa Neto ila ukakosa kuonekana wazi machoni pa wasaidizi wa refa katika mechi ya La Liga iliyopigwa mnamo Novemba 26, 2017.

Tukio hilo ni moja kati ya sababu ambazo kwa sasa zimewachochea vinara wa soka ya Uhispania kuanzisha upya mjadala kuhusu uwezekano wa kushirikisha teknolojia (VAR) katika michuano yao ya baadaye kama ilivyo katika Ligi Kuu nyinginezo za bara Ulaya. 

“La Liga ni miongoni mwa ligi zinazojivunia huduma za wachezaji wa haiba kubwa zaidi duniani. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba kivumbi kinachowapa hifadhi masogora wenye majina makubwa ya kutajika kufu ya Messi na Cristiano Ronaldo hakijakumbatia suala la teknolojia,” akasema kiungo wa Barcelona, Sergio Busquets katika mawazo yaliyoungwa mkono na kocha msaidizi wa Valencia, Ruben Uria.

Kwa mujibu wa Suleiman Waberi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Marefa wa CAF, teknolojia ya VAR itaanza kushirikishwa katika fainali za CHAN mwakani kwenye hatua ya robo-fainali kwa nia ya kupunguza utata katika mengi ya maamuzi ya marefa.

“Teknolojia itakuwa sehemu muhimu katika maamuzi ya marefa mechi za CHAN 2018 zitakapoingia hatua ya nane-bora. Michuano inayoingia katika awamu hiyo inastahili kusimamiwa kwa uangalifu zaidi ili kupunguza makosa ya wazi ambayo vinginevyo yana uwezo wa kushusha hadhi ya kipute chenyewe,” akasema Waberi.

Kivumbi hicho cha mataifa 16 kimeratibiwa kutandazwa katika miji ya Casablanca, Marrakech, Tangiers na Agadir nchini Morocco kati ya Januari 13 na Februari 4.

Japo matumizi ya VAR si sehemu ya mahitaji ya kimsingi kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Waberi anahisi kwamba yapo maamuzi manne muhimu ambayo refa anaweza kuyafikia katikati ya uwanja kupitia msaada wa teknolojia hiyo.

“Refa atakuwa katika nafasi murua ya kuagiza wasaidizi wake kurejelea video za VAR kubaini uhalali na uharamu wa bao, mchezaji anayestahili kuadhibiwa baada ya makabiliano, uhalali na uharamu wa penalti na makosa madogo ambayo si rahisi kuonekana machoni pa refa aliye katikati ya uwanja.”

Mshindi wa Kombe la CHAN 2018 atatia kapuni kima cha Sh125 milioni tofauti na Sh75 milioni ambazo DR Congo walituzwa kutokana na ufanisi waliojivunia jijini Kigali, Rwanda mnamo 2016.

Kwenye droo ya fainali za mwaka ujao, Nigeria wamepangwa katika kundi moja na mabingwa wa zamani wa Kombe la CHAN Libya, Rwanda na Equatorial Guinea kwenye Kundi C. Nigeria waliomaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za CHAN 2014 walibanduliwa katika hatua ya makundi kwenye kipute kilichoandaliwa Rwanda mnamo 2016.

Kundi A linawajumuisha Morocco, Guinea, Sudan na Mauritania huku Kundi B likiwashirikisha Ivory Coast, Zambia, Uganda na Namibia. Angola, Cameroon, Congo Brazzaville na Burkina Faso wanakamilisha Kundi D.

 
KUNDI A (Casablanca): Morocco, Guinea, Sudan, Mauritania.
KUNDI B (Marrakech): Ivory Coast, Zambia, Uganda, Namibia.
KUNDI C (Tangier): Libya, Nigeria, Rwanda, Equatorial Guinea.
KUNDI D (Agadir): Angola, Cameroon, Congo Brazzaville, Burkina Faso.