Malkia Strikers yatumia Ethiopian Airlines badala ya KQ

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  14:09

Kwa Muhtasari

Wakenya wamesikitishwa na serikali kutotilia maanani ahadi ya timu za taifa za Kenya kutumia ndege za Kenya Airways kwa safari za kimataifa.

 

WAKENYA wamesikitishwa na serikali kutotilia maanani ahadi ya timu za taifa za Kenya kutumia ndege za Kenya Airways kwa safari za kimataifa.

Mwezi mmoja tu baada ya serikali kuzindua mpango wa Sh4 bilioni wa kutumia ndege za Kenya Airways kusafirisha timu za taifa, maswali yameibuka kuhusu mpango huo. Malkia Strikers imetumia ndege ya Ethiopian Airlines kuelekea Cameroon, Alhamisi.

Vyombo vya habari nchini Kenya vilitangaza Septemba 9, 2017 kuwa serikali imeingia katika mapatano ya mwaka mmoja ya Sh4 bilioni na Kenya Airways kusafirisha timu za taifa.

Katika hafla hiyo jijini Nairobi, Katibu kutoka Wizara ya Michezo, Peter Kaberia, alisema, “Michezo nchini Kenya ni fahari kubwa na itakuwa heshima kubwa wanamichezo wetu wakitumia ndege za Kenya Airways.”

Hata hivyo, baada ya Malkia Strikers kuelekea Cameroon ikitumia Ethiopian Airlines ya nchi ya Ethiopia kwa mashindano ya Afrika yatakayotumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika mashindano ya dunia, Wakenya wengi wameelezea masikitiko yao.

Katika mtandao wake wa kijamii, Jose Emba, alisema, “Inasikitisha kuwa timu yetu ya taifa inatumia Ethiopian Airlines. Nakumbuka tulikuwa na mpango wa ndege za Kenya Airways kutumiwa na timu za taifa na sielewi kinachoendelea. Sielewi kwa nini Malkia Strikers inapitia jijini Addis Ababa nchini Ethiopia na kuna ndege za Kenya Airways za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi nchini Cameroon. Ninavyoelewa ni kuwa timu ya taifa inawakilisha taifa. Nakumbuka mwezi mmoja uliopita, Wizara ya Michezo ilisema timu zote za taifa zitakuwa zikitumia ndege ya kitaifa.”

Naye Alex Tarre aliikashifu Malkia Strikers. “Timu ya taifa inakataa kutumia ndege ya kitaifa na badala yake inakimbilia kwa mshindani, na inatarajia kupata ufadhili kutoka kwa ndege ya kitaifa. Hilo hufanyika tu Kenya pekee…Hata hivyo, kila la kheri Malkia Strikers.”