http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564786/medRes/1974960/-/lmepwk/-/robanyo.jpg

 

Mancini apewa majukumu Azzuri aifufue

Roberto Mancini

Kocha mpya wa Italia, Roberto Mancini, azungumza na wanahabari Mei 15, 2018, katika kituo cha mazoezi cha Coverciano karibu na Florence. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  14:39

Kwa Muhtasari

Kocha wa zamani wa Inter Milan na Manchester City, Roberto Mancini anakabiliana na kibarua kizito cha kuirudisha timu ya Taifa ya Italia ‘Azzuri’ kwenye mstari baada ya juzi kutangazwa kama kocha mkuu akirithi mikoba ya Gian Piero Ventura aliyeshindwa kuiongoza timu hiyo kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Juni-Julai 2018 nchini Urusi.

 

ROME, Italia

KUTEULIWA kwa Kocha Roberto Mancini kunamaliza sintofahamu ya miezi sita juu ya nani hasa angepewa kibarua cha kurudisha heshima ya Italia iliyoshindwa kufuzu Kombe la Dunia chini ya Ventura aliyetimuliwa Novemba. Italia ilishiriki mfululizo kwa miaka 60 tangu mwaka 1958.

Majina kadhaa yalikuwa yakitajwa kupewa jukumu hilo, miongoni mwao akiwemo Mancini mwenyewe, kocha wa Chelsea, Antonio Conte pamoja na Carlo Ancelloti ambaye kwa sasa hana timu.

Kibarua cha kwanza kwa Mancini, ambaye kabla ya kupewa jukumu hilo alikuwa akiinoa timu ya Zenith St. Petersburg ya Urusi, ni kuhakikisha Italia inafuzu kwenye mashindano ya Ulaya mwaka 2020.

Mancini ni miongoni mwa makocha wanaoheshimika nchini Italia kutokana na mafanikio aliyopata katika klabu mbalimbali alizoziongoza ikiwa ni pamoja na kutwaa Kombe la Coppa Italia akiwa na Fiorentina mwaka 2001, kuiongoza Inter Milan kutwaa Ubingwa wa Italia kwa misimu mitatu mfululizo pamoja na kutwaa taji la Ligi Kuu England na Kombe la FA England akiwa na Manchester City.