Mandela aiomba Martizburg imwachilie mwishoni mwa 2017

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:30

Kwa Muhtasari

BEKI matata wa Harambee Stars, Brian Mandela yuko pua na mdomo kupata hifadhi mpya kambini mwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini siku chache baada ya kuwaomba waajiri wake, Martizburg Utd kumwachilia rasmi mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.

 

Chini ya kocha mzawa wa Serbia ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Uganda Cranes, Milutin Sredojevic Micho, Pirates wanasaka uthabiti utakaowatambisha zaidi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) msimu huu.
Mapema Agosti 2017, Mandela ambaye alihusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Mamelowdi Sundowns aliomba uraia wa Afrika Kusini. 

Ingawa hatakuwa na uwezo wa kuisakatia timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Bafana Bafana’ hata iwapo ombi lake litaidhinishwa mwishoni mwa mwaka huu, kiini cha Mandela kutaka kuwa raia wa taifa hilo ni kujipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha klabu yoyote itakayomsajili kwa lengo la kunogesha kampeni za Ligi Kuu ya PSL.

Kwa mujibu wa sheria zinazodhibiti soka inayopigwa na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya PSL, idadi kubwa zaidi ya wachezaji wa kigeni ambao timu inaweza kusajili kwa msimu mmoja ni masogora watano huku kila klabu ikiwa na idhini ya kuwawajibisha jumla ya wachezaji watatu pekee kwenye kikosi cha kwanza katika kila mchuano.

Hii ni ‘dhiki’ ambayo Mandela ataepuka iwapo atajipa uraia wa Afrika Kusini. Kwa kuwa hatua hiyo itamweka katika hali ya kuwa raia wa mataifa mawili, beki huyo atakuwa huru kuendelea kuvalia jezi za Harambee Stars, kikosi ambacho kimekuwa kikitegemea pakubwa huduma zake katika miaka ya hivi karibuni.

Mandela, 23, amekuwa kivutio kwa klabu nyingi maarufu ndani na nje ya Afrika Kusini baada ya kujivunia msimu wa kuridhisha kambini mwa waajiri wake wa sasa msimu huu.

Katika mojawapo ya hatua za kujipa uhakika wa kuendelea kujivunia utajiri wa kipaji cha Mandela, Maritzburg walirefusha muda wa kuhudumu kwa nyota huyo kambini mwao kwa miaka mitano mwanzoni mwa mwaka huu katika maelewano ambayo yatamshuhudia akiwasakatia hadi Juni 2019.  

Kibarua kigumu ambacho kwa sasa kinawakosesha usingizi vinara wa Maritzburg ni jinsi ya kumzuia Mandela kutua Sundowns au Pirates ambao kwa mujibu wa kocha Fadlu Davids wamekuwa wakimvizia beki huyo kwa muda mrefu.

Mnamo Julai 2012, vinara wa Santos FC walifikia maelewano na mabingwa mara 11 wa taji la Ligi Kuu ya KPL, Tusker FC kuzitwaa huduma za Mandela. Katika maafikiano hayo, Mandela aliwaonesha mgongo waajiri wake hao kwa kutia saini mkataba wa miaka mitatu.