Mapokezi ya kufana kwa Simbas licha ya matokeo duni

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, November 20  2017 at  17:22

Kwa Muhtasari

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya wanaume ya Kenya imerejea nchini kutoka Hong Kong, Jumatatu.

 

Simbas, inavyofahamika kwa jina la utani, imepata mapokezi ya kufana ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kiamsha kinywa katika hoteli ya kifahari ya EKA jijini Nairobi.

Vijana hao wa Kocha Jerome Paarwater watapumzika majuma mawili kabla ya kurejelea mazoezi katika klabu zao zinazojiandaa kumenyana katika Ligi Kuu itakayoanza Novemba 25, 2017.

Katika ziara yake ya Hong Kong kwa shindano la Cup of Nations, Simbas ilikaribishwa na kipigo cha alama 23-3 na Chile hapo Novemba 10. Ilipapurwa 31-10 katika mechi yake ya pili dhidi ya Urusi mnamo Novemba 14 kabla ya kukamilisha kampeni kwa kulemwa 40-30 na wenyeji Hong Kong hapo Novemba 18.

Urusi ilihifadhi taji baada ya kupepeta Hong Kong 16-13, Kenya (31-10) na Chile (42-11). Ilimaliza shindano kwa alama 14. Hong Kong ilishikilia nafasi ya pili kwa alama 10 ilizopata kwa kuchapa Chile 13-6 na Kenya 40-30.

Chile ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa alama tano nayo Kenya ikavuta mkia kwa alama moja. Ilikuwa mara ya pili Kenya ilishiriki shindano hili baada ya kumaliza makala ya mwaka 2011 katika nafasi ya pili nyuma ya Hong Kong.