FIFA yapiga faini mataifa 6 ya Afrika kwa kuvunja sheria za soka

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  18:48

Kwa Muhtasari

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limetoza faini mataifa sita ya Afrika jumla ya Sh8, 375, 780 kwa uvunjaji wa sheria wakati wa mechi zao za wanaume za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwezi Septemba 2017.

 

Super Eagles ya Nigeria ndiyo imepokea adhabu kali (Sh3,094,500) ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Sh2,063,000), Mali (Sh1,547,250), Zambia (Sh722,050), Gabon (Sh639,530) na Morocco (Sh309,450).

Nigeria iliadhibiwa kwa sababu mashabiki wake waliingia uwanjani ilipobwaga Indomitable Lions ya Cameroon 4-0 mjini Uyo mnamo Septemba 1 katika mechi ya kundi B.

DR Congo ilipokea adhabu yake baada ya mashabiki wake kuzua vurugu na kurusha chupa na fataki uwanjani baada ya timu yao kukabwa 2-2 na Tunisia katika mechi ya kundi A mnamo Septemba 5 jijini Kinshasa.

Mashabikiwa Mali walitupa chupa na viti uwanjani wakati wa mechi dhidi ya Morocco ambayo timu hizi hazikufungana bao mnamo Septemba 5 jijini Bamako. Morocco ilipigwa faini ya Sh309,450 kwa sababu mashabiki wake walipuliza vipenga wimbo wa taifa wa Mali ukichezwa mnamo Septemba 1. Morocco ilishinda mechi hiyo 6-0 jijini Rabat.

Zambia ilitozwa faini baada ya mashabiki wake kurusha vitu mbalimbali uwanjani timu yao ya Chipolopolo ilipoiponda Algeria 3-1 jijini Lusaka mnamo Septemba 2.

Gabon ilipoteza mechi dhidi ya Ivory Coast kwa mabao 3-0 na kupigwa faini ya Sh639, 530 kwa sababu ya kuchezesha kiungo Merlin Tandjigora licha ya kuwa alikuwa anatumikia marufuku kutokana na kadi alizolishwa. Gabon haikupoteza pointi yoyote kutoka mechi hiyo kwa sababu ilikuwa imelimwa 3-0.

Senegal na Burkina Faso zilikwepa adhabu yoyote, lakini zikaonywa kwa kuanza mechi baina yao zikiwa zimechelewa jijini Dakar na tena jijini Ouagadougou.

FIFA imetangaza Alhamisi pia imepiga Equatorial Guinea marufuku kushiriki Kombe la Dunia la wanawake mwaka 2019 na kuitoza faini ya Sh10, 553,453 baada ya kuchezesha wachezaji 10 katika mechi ya kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2016 wasiostahili.

Wachezaji wengine wawili Muriel Linda Mendoua Abessolo na Francisca Angue Ondo Asangono waliotumia stakabadhi za uongo wamepigwa marufuku mechi 10.