Mbao yajiuliza itoke vipi Ligi Kuu

Na WAANDISHI WA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  12:08

Kwa Muhtasari

Baada ya kupokea kipigo kutoka kwa Azam, timu ya Mbao imesema inapitia kipindi kigumu lakini itakaa sawa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

BAADA ya kupokea kipigo kutoka kwa Azam, timu ya Mbao imesema inapitia kipindi kigumu lakini itakaa sawa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kauli hiyo imetolewa na nahodha wa Mbao Yusuph Ndikumana muda mfupi baada ya kulala mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam juzi usiku.

Ndikumana alisema ‘mambo’ ni magumu lakini hawatakata tamaa kwa kuwa wana michezo mingi ya kuamua hatma ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Mbao imeshindwa kutamba msimu huu na katika michezo sita iliyopita imeambulia pointi moja na vipigo katika michezo mitano.

Mara ya mwisho Mbao ilipata ushindi Februari 4 ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

"Inaumiza lakini inabidi tukubali matokeo  timu inapitia kipindi kigumu ni kama mbaya unatupitia ila hatupaswi kukata tamaa na kurudi nyuma. Bado tuna nafasi ya kujiuliza tumekosea wapi ili tujirekebishe," alisema Ndikumana.

Mchezaji huyo alisema wachezaji wana nafasi ya kufanya vyema katika michezo ijao ya ligi baada ya kubaini kasoro ambazo watazifanyia kazi kambini.

Na Oliver Albert, Mwananchi oalbert@mwananchi.co.tz

CDA yagonga mwamba Sita Bora

Dodoma. Timu kongwe ya CDA Dodoma imeshindwa kupenya katika hatua ya fainali ya Sita Bora mkoani hapa.

Katika hatua ya awali ya Ligi ya Mkoa Dodoma iliyopigwa kwenye vituo tofauti, timu sita kati ya 15 CDA ilishindwa kufua dafu.

Awali, CDA iliyowahi kucheza Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu) ilipewa nafasi ya kung’ara katika ligi hiyo kutokana na uzoefu wake.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa Dodoma (Dorefa) Hamisi Kissoy alisema ligi ya hatua sita bora inatarajiwa kuanza Machi 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Kiongozi huyo alisema timu zilizopenya katika hatua hiyo zimepewa nafasi ya kuongeza wachezaji watano ambao hawakucheza kwenye michezo ya hatua ya awali.

Na Mateleka Jalilu

 

ZFA yazishusha daraja timu tatu

Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini Magharibi, Unguja imezishusha daraja timu tatu za Ligi Daraja la Pili na Tatu Kanda ya Unguja.

Timu hizo Gereji, Kilimani Stars za Daraja la Pili na Chumbuni ya Daraja la Tatu baada ya klabu hizo kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Katibu Mkuu wa ZFA Wilaya Mjini Yahya Juma Ali, alisema klabu hizo zilionyesha utovu wa nidhamu kwa kuwapiga waamuzi katika mechi zao.

“Uamuzi wa kuzishusha daraja umetolewa baada ya Kamati ya Wilaya ya Mjini Magharibi kujiridhisha timu hizo zimeonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu kuanzisha vurugu hadi kupigwa wamuzi,” alisema Ali.

Na Haji Mtumwa

 

Forest kuivaa Uzunguni Fainali Ligi Mkoa

Kilimanjaro: Timu ya Forest imetinga fainali ya Ligi Daraja la Tatu Ngazi ya Mkoa baada ya kuichapa Goldern Heroes mabao 3-0 kwenye Uwanja wa CCM.

Katika mchezo wa fainali ya kwanza, Uzunguni ilifuzu fainali baada ya kuilaza Upendo kutoka Wilaya ya Siha bao 1-0.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro Mohammedi Mussa alidai mchezo wa fainali utapigwa Jumamosi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira atarajiwa kuwa mgeni.

“Mchezo huo utatoa bingwa wa mkoa msimu huu ambaye ataanza kujiandaa na mashindano ya Ligi ya Mabingwa ya Mikoa (RCL) itakayoanza mwanzoni wa mwezi ujao” alisema Mussa.

Na Yohana Challe