Mbinu za Okumbi za ukufunzi ni duni ajabu - Abbas

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:21

Kwa Mukhtasari

ALIYEKUWA kipa mahiri wa Harambee Stars, Mahmoud Abbas almaarufu ‘Kenyan One’ amemsuta pakubwa kocha Stanley Okumbi kwa mazoea ya kubadilisha kikosi chake cha kwanza kila mara katika vibarua tofauti. 

 

Kwa mujibu wa Abbas, kubadilishwa mara kwa mara kwa wachezaji wanaounga kikosi cha Stars kunachangia pakubwa kusambaratika kwa timu.

Aidha, amewataka wachezaji wa timu ya taifa kujituma maradufu na kutawaliwa na hamasa ya kuwakilisha kikosi vilivyo katika majukwaa mbalimbali ya soka ya kimataifa.

Kauli ya Abbas inajiri siku chache baada ya Stars kupoteza michuano miwili ya kupimana nguvu dhidi ya Iraq (2-1) na Thailand (1-0).

“Mabadiliko ya kila mara yanakosesha vijana fursa ya kuoanisha mtindo wao wa kucheza. Uthabiti wa timu hupotea na viwango vya ubora kushuka,” akatanguliza Abbas huku akisisitiza haja ya Okumbi kuteua wachezaji atakaokuwa na uhakika wa kuwadumisha kikosini kwa muda mrefu.

“Okumbi amedhibiti mikoba ya Stars kwa muda mrefu sasa. Anastahili kufikia sasa awe anafahamu ukubwa wa uwezo wa kila mchezaji, ajue masogora wa kutegemewa katika kila kibarua na nyota ambao wana uhakika wa kuunga kikosi cha wachezaji 11-bora,” akaongeza.

Mbali na kuwataka vinara wa FKF kufanyia benchi la ufundi la Stars mabadiliko muhimu, Abbas pia amewahimiza wachezaji kujitolea kwa dhati kukiwakilisha kikosi kwa imani kwamba hatua hiyo itawaboresha zaidi kitaaluma na kurejesha Kenya katika ramani ya soka ya Afrika na dunia.

Stars walitumia michuano hiyo miwili ya kirafiki wiki jana kama sehemu ya maandalizi ya kumenyana na Ghana kwenye mechi ya Kundi F ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2019 nchini Cameroon.