Mechi ya Ingwe dhidi ya SoNy yahamishiwa Kericho Green

Na  GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, September 11  2017 at  15:26

Kwa Mukhtasari

MECHI kati ya AFC Leopards na SoNy Sugar imehamishwa na Kampuni inayoendesha Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (KPL) kutoka uwanja wa Afraha mjini Nakuru hadi uwanjani Kericho Green mjini Kericho.

 

Leopards, ambayo imeshinda ligi mara 13, ilipangiwa kukaribisha mabingwa wa mwaka 2006, SoNy Sugar uwanjani Afraha saa nane mchana Jumatano. Uwanja wa Afraha sasa haupatikani.

Mechi kati ya mabingwa wa mwaka 2009, Sofapaka na mabingwa mara nne Ulinzi Stars, ambao uwanja wao wa nyumbani huwa Afraha, pia imehamishiwa mjini Kericho.

Ulinzi iliratibiwa kualika Sofapaka uwanjani Afraha saa kumi na robo Jumatano. Saa ya mechi haijabadilishwa.

Katika mechi hizo, Leopards italenga kuimarisha rekodi ya kutoshindwa hadi mechi nne. Itaingia mchuano huu na motisha ya kupepeta Zoo Kericho 3-1 Jumapili.

Uwanja wa nyumbani wa Zoo ni Kericho Green. SoNy pia ilipata motisha kubwa kabla ya mechi ya Ingwe iliponyuka mabingwa watetezi Tusker 2-0 mjini Awendo mnamo Jumapili.

Leopards na SoNy zinashikilia nafasi za 13 na 14 kwenye jedwali la ligi hii ya klabu 18. Zimezoa pointi 27 na 26, mtawalia. Zilikutana mara ya mwisho katika mechi ya mkondo wa kwanza msimu huu ambapo SoNy iliwika 1-0 mwezi Mei.

Tangu mwaka 2014, Leopards na SoNy zimekuwa na mtindo wa kuzoa pointi tatu kutoka kwa mwenzake. Swali, zinapojiandaa kukabiliana ni je, mtindo huo utaendelea?

Nambari mbili Sofapaka na Ulinzi, ambayo iko katika nafasi ya sita, zitakabana koo, huku Sofapaka ikisaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya wanajeshi hawa baada ya kupoteza mechi mfululizo.

Ulinzi iliibuka na ushindi wa 1-0 ugenini mwezi Mei na itapimwa uwezo wake dhidi ya Sofapaka ambayo imeamka sana.