http://www.swahilihub.com/image/view/-/5151506/medRes/2367617/-/vqfxca/-/mkufunzi+pic.jpg

 

Mkufunzi Fiba aitabiria makubwa wavu

Na Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi co.tz

Imepakiwa - Monday, June 10  2019 at  12:31

 

Dar es salaam. Mkufunzi wa Chama cha Wavu cha Kimataifa (Fiba), Tony Westman raia wa Sweden ameutabiria mafanikio mchezo wa Wavu nchini.

Westman ambaye amewanoa makocha 29 waliohitimu mafunzo ya kimataifa ya levo ya kwanza Jana Jumapili alisema, Tanzania inanafasi ya kufanya vizuri kimataifa kwenye mchezo wa wavu kama wataamua.

"Wavu ni mchezo rahisi kuchezwa mahali popote, hivyo ni jukumu la ninyi makocha kubadilisha upepo wa mchezo huu ili Tanzania iwe tishio kimataifa," alisema Westman wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Filbert Bayi, Kibaha Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya siku 11 yaliandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na kudhaminiwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kupitia kitengo chake cha misaada (OS).

Mwakilishi wa TOC, Irene Mwasanga alisema hiyo ni mara ya tatu Kamati yao kutoa mafunzo kwenye chama cha mpira wa Wavu nchini.

"Awali ilikuwa mwaka 2006 na matunda ya mafunzo ya mwaka huo yameonekana ambapo mmoja wa washiriki  katika mafunzo hayo (Fred Selengia) alijiendeleza na sasa ni mkufunzi wa Fiba,".

Mafunzo mengine ya wavu yalifanyika mwaka 2013 na mwaka huu ambapo makocha 23 wanaume na sita wanawake wamehitimu.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya makocha nchini, Dismas Amir alisema mafunzo hayo yamepanua wigo kwa mchezo wa wavu nchini.