http://www.swahilihub.com/image/view/-/5127996/medRes/2352168/-/ws5xqy/-/mo+pic.jpg

 

Mo: Sijatoa Sh20 Bil Simba

Na Majuto Omary,momary@tz.nationmedia.com

Imepakiwa - Thursday, May 23  2019 at  11:35

 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji  ‘Mo’ amesema hajatoa fedha za uwekezaji Sh20 bilioni, alizoahidi kutoa baada ya kushinda zabuni.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dewji alisema kuwa hajatoa fedha za uwekezaji ndani ya klabu hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo urasimishaji.

Dewji alisema Simba haikuwa na nyaraka halisi za mali zake yakiwemo majengo na Uwanja wa Bunju, hivyo uongozi ulilazimika kufanya kazi ya ziada kupata hati halisi kwa mujibu wa sheria hatua iliyochelewesha mchakato wa uwekezaji.

 “Simba ilikuwa na madeni Mamlaka ya Mapato (TRA), klabu ilitakiwa kupeleka hesabu kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu. Kwa sasa zoezi hilo limekamilika na hata hati halisi za mali ya klabu (majengo na viwanja)  limekamilika, mchakato wa kufanikisha zoezi la uwekezaji limekamilika,” alisema Dewji.

Mkurugenzi huyo alisema anatarajia kuanza kutoa fedha zilizomo ndani ya mkataba wa uwekezaji muda mfupi ujao kwa kuwa mchakato wa uwekezaji umekamilika.

Pamoja na kutokamilika kwa mchakato huo, Dewji alidai alikuwa akitoa fedha za maendeleo ya klabu hiyo ikiwemo suala la usajili na mambo mengine ya uendeshaji wa klabu.

Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Swedi Mkwabi alisema ana matumaini timu yao msimu ujao itakuwa tishio katika mashindano mbalimbali, baada ya mchakato wa uwekezaji kukamilika.

Dewji aliyeshinda zabuni, alikubali kutoa Sh20 bilioni kupata asilimia 50 ya hisa ingawa Serikali ilisisitiza kwa utaratibu mpya anatakiwa kupewa asilimia 49 na nyingine 51 zitakwenda kwa wanachama.

Katika ahadi zake Dewji aliahidi ujenzi wa viwanja viwili vya mazoezi ambapo kimoja kitakuwa cha nyasi bandia na nyasi za kawaida.

Pia aliahidi ujenzi wa hosteli yenye vyumba 35, ujenzi wa mgahawa na eneo la kujiburudisha kwa wachezaji, studio ya kuzalisha vipindi vya televisheni vya Simba, ‘gym’ na akademia za timu za vijana ili kupata wachezaji wa kuuza ndani na nje ya nchi.

Usajili

Dewji alisema atakuwa tayari kumnunua mchezaji atakayependekezwa na benchi la ufundi kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema atatumia zaidi ya bajeti ya msimu uliopita ambayo ilifikia Sh1.3 billioni kusajili wachezaji ambao wameleta mafanikio msimu huu.

Dewji alisema anataka klabu hiyo kuingia katika vita ya usajili na timu kubwa kama TP Mazembe ya DR Congo, Zamaleki, Al Ahly za Misri na klabu nyingine bora Afrika.

Benchi la Ufundi

Dewji alisema ataboresha benchi la ufundi kwa kuongeza mtaalamu wa tiba kwa wachezaji ana anatarajia kumuongeza mkataba kocha Patrick Aussems.

Alisema anatarajia kukutana na Aussems wiki hii kujadili mkataba wake na masuala mengine ya masilahi ili Simba kuwa timu bora Afrika.

Kambi Marekani

Bilionea huyo wa Tanzania alisema  bodi ya wakurugenzi imepanga kuipeleka Simba Marekani na Ureno kuweka kambi ya kujiandaa na mechi za msimu ujao wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Pikipiki

Dewji ametoa zawadi ya pikipiki aina ya ‘boxer’ kwa wachezaji zenye thamani ya Sh 2.4 baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

“Nimefarijika kwa mafanikio ya timu ambayo yametokana na umoja ndani ya klabu baada ya kuanza mfumo mpya wa uongozi,” alisema Dewji.