Mourinho awashika uchawi nyota wake

Kocha Jose Mourinho  

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  08:56

Kwa Muhtasari

Ni vizuri kuwaruhusu kuondoka kuliko kucheza chini ya kiwango

 

Manchester, England. Baada ya Manchester United kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Arsenal kwenye Uwanja wake wa Old Trafford, Kocha Jose Mourinho amewatupia lawama wachezaji.

Pamoja na Mourinho kukasirika lakini ameendeleza rekodi nzuri mbele ya Arsenal kwa kuwa katika mechi 16 za Ligi Kuu alizokutana nayo amepoteza mchezo mmoja tu, ameshinda saba na kutoka sare michezo minane.

Kilichomfanya Mourinho kukasirika ni kuona ahadi yake ya kumaliza ndani ya nne bora ikianza kuonekana ni ndoto baada ya kushuka hadi pointi nane chini ya Chelsea inayoshika nafasi ya nne ambayo ni ya mwisho ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Kilichotufanya tushindwe mchezo huu ni kutokana na baadhi ya wachezaji wetu kutotimiza wajibu wao, nafikiri sasa ni vizuri kuwaruhusu kuondoka kuliko kucheza chini ya kiwango,” alisema kocha huyo kwa hasira.

Ingawa hakumtaja mchezaji yeyote jina, lakini inadhaniwa aliwalenga Paul Pogba na wengine ambao katika siku za hivi karibuni amekuwa na msuguano nao wa mara kwa mara akiwashutumu kucheza chini ya kiwango.

Kwa kocha wa Arsenal, Unai Emery baada ya kufungwa na Man City na Chelsea katika mechi mbili za kwanza amezidi kuimarika kwa kuwa hajapoteza mechi 20 mfululizo na tayari anaonekana kutokuwa na presha.