http://www.swahilihub.com/image/view/-/4692222/medRes/2065331/-/pmm4ak/-/testi.jpg

 

Msola, Kibadeni wampa neno Aussems

Patrick Aussems

Kocha wa Simba Patrick Aussems. Picha/HISANI 

Na THOBIAS SEBASTIAN, Mwananchi

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  14:45

Kwa Muhtasari

Makocha wakongwe nchini Tanzania, Mshindo Msola na Abdallah Kibadeni wamemtaka kocha wa Simba Patrick Aussems kuongeza nguvu kwa kusajili wachezaji wa safu ya ulinzi ili kuimarisha kikosi hicho.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

MAKOCHA nguli, Dkt Mshindo Msola na Abdallah Kibadeni, wamemtaka Patrick Aussems kuimarisha safu ya ulinzi na siyo mshambuliaji au kiungo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Msola na Kibadeni walidai Simba ina tatizo kubwa katika nafasi ya ulinzi na siyo kiungo au mshambuliaji kama anavyodai Aussems.

Aussems, aliwahi kukaririwa akisema anataka kuongeza ‘nyota’ wawili wa kigeni katika nafasi ya mshambuliaji na kiungo katika usajili wake.

Tayari Simba inawafanyia majaribio wachezaji wanne wa kigeni Sadney Urikhob wa Namibia, Kissimbo Hunlede (Togo), Moro Lamine (Ghana) na Sean Ourega.

Wakati Simba ikiwafanyia majaribio wachezaji hao, makocha nchini wameipa angalizo katika usajili wanaotaka kuufanya huku wakisisitiza, Simba haina tatizo la mshambuliaji wala kiungo, inahitaji kuongeza mabeki.

"Nikitazama Simba naona inahitaji kuongeza mabeki watatu si washambuliaji, tangu alipoumia (Shomari) Kapombe hakuna mtu wa kuziba pengo lake,” alisema Kibadeni.

Kocha huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alidai Aussems anatakiwa kupata beki mwingine wa kati mwenye kiwango bora kuwazidi Juuko Murshid na Pascal Wawa.

Dkt Msola alisema Simba imekuwa ikifanya makosa mengi katika eneo la ulinzi ambalo lipaswa kufanyiwa kazi mapema wakati timu hiyo inajiandaa kwa mechi tatu dhidi ya Al Ahly ya Misri (mechi mbili) na JS Saoura ya Algeria.

Safu ya Ulinzi ya Simba inaundwa na mabeki Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Juuko Murshid.